China sambamba na kuashiria kuidhinishwa kanuni mpya na baraza la mawaziri la usalama la Israel ili kuimarisha udhibiti wa Ukingo wa Magharibi, imeonya kuhusu matokeo mabaya ya hatua hiyo.
Lin Jian, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, ametoa radiamali hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari na kusema: “Gaza na Ukingo wa Magharibi zote ni sehemu zisizoweza kutenganishwa za eneo la Palestina, na suluhisho la mataifa mawili ndiyo njia ya msingi ya kutatua suala la Palestina.”
Lin Jian aliongeza: “China imekuwa ikipinga ujenzi wa vitongoji vipya katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa na jaribio lolote la kunyakua au kuvamia ardhi za Palestina na kudhoofisha msingi wa kisiasa wa suluhisho la mataifa mawili.” Kadhalika alionya kuhusu hali tete katika Ukanda wa Gaza, akisisitiza kwamba pande husika zinapaswa kujiepusha na vitendo vitakavyozidisha tofauti na kuongeza mvutano.
Matamshi ya afisa huyo wa China yanatolewa baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Palestina kutangaza hapo awali katika taarifa kwamba, makubaliano ya baraza la mawaziri la Israel na mapendekezo ya Waziri wa Vita Israel Katz na Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich kuhusu ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi hayakubaliki.
Kwa mujibu wa ripoti, mawaziri wa ulinzi na fedha wa utawala vamizi wa Israel wanaelekea kuidhinisha mfululizo wa maamuzi ili kuimarisha unyakuzi wa ardhi za Ukingo wa Magharibi. Maamuzi haya yatafanya mabadiliko makubwa katika mifumo ya ardhi na taratibu za ununuzi wa ardhi, na yatawaruhusu wavamizi kubomoa majengo yanayomilikiwa na Wapalestina katika Eneo la “A.” Utekelezaji wa maamuzi haya utasababisha upanuzi mkubwa wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi.

Maeneo ya “A” katika Ukingo wa Magharibi ni sehemu ya mgawanyiko wa kiutawala na usalama wa eneo linalokaliwa kwa mabavu kwa kuzingatia Makubaliano ya Oslo kati ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na utawala ghasibu wa Israel katika miaka ya 1990. Kulingana na mipango hii, Ukingo wa Magharibi uligawanywa katika maeneo matatu, A, B, na C. Katika maeneo ya “A”, usimamizi wa masuala ya kiraia na udhibiti wa usalama wa ndani uko chini ya udhibiti kamili wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Hii ina maana kwamba polisi wa Palestina wanawajibika kwa usalama wa kila siku, na usimamizi wa huduma za manispaa, elimu, afya, na masuala ya kiutawala pia unafanywa na taasisi za Palestina. Katika maeneo ya A, utawala wa Kizayuni na Wayahudi hawana haki ya kutumia uhuru na uwepo ndani yake. Hata hivyo, wanajeshi wa Israel na walowezi wenye misimamo ya kuchupa mipaka wanaendelea kuwanyanyasa Wapalestina kwa uwepo wao katika maeneo haya. Kijiografia, maeneo ya “A” yanajumuisha hasa miji mikubwa ya Palestina na vituo vya idadi kubwa ya watu, ikiwa ni pamoja na Ramallah, Nablus, Jenin, Tulkarm, Qalqilya, Beit Lahm, na sehemu kubwa ya al-Khalil. Maeneo haya yanaunda takriban asilimia 18 ya eneo lote la Ukingo wa Magharibi, lakini ni makazi ya sehemu kubwa ya wakazi wa Palestina.
Msimamo wa ukosoaji mkali wa China katika kukabiliana na vitendo vipya vya Israel katika Ukingo wa Magharibi mnamo Februari 2026 unategemea sababu kadhaa muhimu:
Kwanza kabisa, China inapinga vikali upanuzi wa vitongoji vipya na majaribio ya kudhibiti zaidi Ukingo wa Magharibi na utawala wa Kizayuni, ikizingatia vitendo hivi kuwa ukiukaji wa sheria za kimataifa. Beijing imesisitiza kwamba, ujenzi na upanuzi wa vitongoji vya Kizayuni katika maeneo yanayokaliwa ni kinyume cha sheria chini ya sheria ya kimataifa na inapinga “jaribio lolote la kunyang’anya” au “uvamizi katika ardhi za Palestina.” Msimamo huu umebainishwa wazi na taarifa rasmi za serikali ya China katika mikutano iliyofanywa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje.

Sababu ya pili muhimu ni kulinda suluhisho la mataifa mawili. China imerudia kusema kwamba suluhisho la kudumu kwa mzozo wa Palestina na Israel ni kupitia kuundwa mataifa mawili huru pamoja, na hatua yoyote inayodhoofisha mchakato wa kisiasa na msingi wa suluhisho hili inachukuliwa kuwa ya uharibifu na hatari. Beijing imesema kwamba upanuzi wa udhibiti wa utawala wa Israel kwa Ukingo wa Magharibi na matokeo yake, hasa katika uwanja wa ujenzi wa vitongoji vya walowezi, unaweza kupunguza uwezekano wa kufikia suluhisho la mataifa mawili na kushadidisha tofauti.
Sababu nyingine ni kwamba, China imeelezea wasiwasi wake kuhusu matokeo ya kibinadamu na haki za binadamu ya vitendo hivi. Ingawa Beijing kwa kawaida haitumii lugha ya haki za binadamu iliyo wazi zaidi ya nchi kama vile nchi za Umoja wa Ulaya katika misimamo yake, misimamo mipya ya China inasisitiza waziwazi kwamba kuimarishwa kwa udhibiti na unyang’anyi wa ardhi dhidi ya Wapalestina kumezidisha kuwa mbaya hali yao ya kibinadamu na kwamba hatua yoyote inayosababisha “kutokuwa na utulivu zaidi” inapaswa kuepukwa.
Kwa kifupi, ukosoaji wa China kwa vitendo vya utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi unatokana na kupinga upanuzi wa vitongoji vya walowezi na unyang’anyi wa ardhi, msisitizo juu ya suluhisho la mataifa mawili, na masuala ya kibinadamu na haki za binadamu, huku wakati huo huo ikijaribu kudumisha taswira yake kama mpatanishi mwenye kujenga katika eneo la Asia Magharibi.