Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Kibu Denis amejiunga na Al Nasr ya Libya baada ya timu hiyo kumnunua kutoka Simba katika dirisha dogo la usajili.

Kibu amefuata nyayo za mshambuliaji mwingine wa Simba, Steven Mukwala ambaye mwezi Januari alijiunga na timu hiyo ya Libya.

Kabla ya kuichezea Simba, Kibu Denis aliwahi kuzitumikia pia Mbeya City, Geita Gold na Kumuyange FC.

Mshambuliaji mpya wa Al Nasr ya Libya, Kibu Denis akiwa gym akifanya mazoezi. Picha na Mtandao

Noti zamvuta

Wahenga walisema fedha ni sabuni ya roho na hilo linaweza kujidhihirisha kwa Kibu Denis namna ambavyo Al Nasr wametumia kiasi kikubwa cha fedha kuhakikisha wanamnasa.

Kibu Denis atavuna kiasi cha Dola 700,000 (Shilingi Bilioni 1.8) katika mkataba wake wa mwaka mmoja na nusu na Al Nasr ya Libya.

Nusu ya fedha hizo, Dola 350,000 (Shilingi milioni 900) ataingiziwa katika akaunti yake moja kwa moja kama dau la ushawishi wa kusaini mkataba.

Nusu iliyobakia ambayo ni Dola 350,000 (Shilingi milioni 900) atakuwa akilipwa kila mwezi kama mshahara na bonasi ambapo kwa mwezi atakuwa akipokea Shilingi milioni 50 za Kitanzania.

Ikumbukwe kwamba Simba yenyewe imepata kiasi cha Dola 300,000 kwa kumuuza mshambuliaji huyo ambaye mkataba wake ulikuwa umebakiza muda wa miezi minne.

Mastaa wamngojea

Kibu Denis anaenda kuwa miongoni mwa nyota kutoka mataifa mbalimbali ambao wanazitumikia timu tofauti zinazoshiriki Ligi Kuu ya Libya.

Mfano wa wachezaji hao ni Fily Traore, Saad Bguir, Thembinkos Lorch, Stephane Aziz Ki, Roger Aholou, Ismail Belkacem, Hamdou El Houni, Yahya Jebrane, Oto John, Nawfel Zerhouin, Ayman Tihar na Ahmed Nasser.

Wengine ni Luis Miquissone, Khadim Diaw, Steven Mukwala, Debora Mavambo, Jean Baleke, Mohamed Zrida, Anatole Abang na Thierry Manzi.

Pia kuna Yakubu Issahaku, Ibrahim Blati Toure, Muaid Ellafi, Pablo Sabbag, Stanley Ogoh, Moussa Benzaid, Ayoub Ayed, Idumba Fasika, Gibril Sillah na Yeison Moreno.

Aliyekuwa mchezaji wa Simba, Kibu Denis ambaye kwa sasa amejiunga na Al Nasr ya Libya. Picha na ,Mtandao

Namba anazoacha

Msimu huu Kibu Denis ameifungia Simba mabao mawili yote yakiwa ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mabao hayo aliyafunga katika mechi ya raundi ya kwanza dhidi ya Nsingizini Hotspurs ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Mshambuliaji huyo anakumbukwa kwa ukame wa mabao ambao aliwahi kuwa nao kwenye Ligi Kuu ambapo alikaa zaidi ya siku 490 bila kufunga bao.

Msimu bila bao

Baada ya Kibu kuifunga Yanga Novemba 5,2023 Kibu akakutanan na ukame mkubwa wa kutoifungia timu yake bao lolote, kila akifanya juhudi za kutafuta bao ilikuwa ngumu kufanikiwa na hatimaye akaumaliza mwaka mzima bila kufunga mpaka alipokuja kucheka na nyavu tena Machi 14,2025 alipokuja kuwafunga Dodoma Jiji mabao mawili akifikisha siku 465 bila ya bao lolote.

Aliyekuwa mchezaji wa Simba, Kibu Denis ambaye kwa sasa amejiunga na Al Nasr ya Libya. Picha na ,Mtandao

Sintofahamu Taifa Stars

Nje ya Simba Kibu alikuwa na utumishi kwenye kikosi cha Taifa Stars lakini miaka ya karibuni alikuwa na matukio yaliyotafsirika kama hakuwa anataka kuichezea timu hiyo akikacha wito wa kujiunga na kikosi hicho mara mbili mfululizo.

Matukio hayo yalikuwa yanawakera mabosi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakiona kama jamaa hajali tena uraia ambao alipewa ambapo wakati Stars inapambana alikuwa akionekana mapumzikoni na familia yake, hata hivyo hivi karibuni alibadilika na kuwa sehemu ya kikosi cha Stars kilichoshiriki Fainali za Mataifa Afrika, kule Morocco ingawa hakupata nafasi kubwa ya kucheza uwanjani.

Presha ya usajili Yanga

Kibu kabla ya kusaini mkataba huuu mpya alikaribia kabisa kusaini Yanga ambayo ilikuwa inafanya juhudi kubwa kumchukua akitokea Simba ambapo alishapewa mpakla mkataba ausome lakini baadaye akachagua kusalia kwa wekundu hao.

Wakati huu Kibu anaondoka Simba kabla ya maamuzi haya, aliwaonya mabosi wa wekundu hao ni bora wafanye biashara na Al Nasser vinginevyo anaweza kwenda Yanga mwisho wa msimu huu, hatua ambayo iliwaamsha viongozi wake na kuamua kuchukua zaidi y ash 700 milioni ili aende huko Libya.

Kibu amemaliza kitabu chake sehemu ya kwanza ndani ya Simba tumuangalie Kimataifa huko Libya kipi kitaendelea kwake, kila la kheri rasta mkandaji.

Aliyekuwa mchezaji wa Simba, Kibu Denis ambaye kwa sasa amejiunga na Al Nasr ya Libya. Picha na ,Mtandao

Makocha wamkubali

Kibu alikuwa na maisha yake yanayoshangaza ambapo hakuna kocha aliyekuja ndani ya klabu hiyo kisha akaamua kwa utashi wake kumweka nje, makocha walikuwa wanamkubali sana wakiona umuhimu wake ndani ya kikosi hicho.

Wakati aliyewahi kuwa kocha wa Simba Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wakati anaanza kazi ndani ya klabu hiyo mapema tu alipoulizwa kuna mchezaji gani amemvutia alitajwa Kibu hatua ambayo iliwashangaza mashabiki wengi ambao walikuiwa hawaoni umhimu wa kiungo huyo.

Makocha wengi walikuwa wanamuona Kibu kama mchezaji ambaye ana mchango mkubwa kwa kuwa na nguvu ya kusukuma mashambulizi na kufanya maamuzi magumu maeneo magumu lakini pia alikuwa na msaada wakati timu haina mpira na wakati inaumiliki, vitu ambavyo kwa macho ya ushabiki ilikuwa ngumu kuonekana umuhimu wake.

Ndani ya Simba Kibu ameondoka akiwa amefunga jumla ya mabao 15 kwenye Ligi Kuu Bara, lakini ndani ya miaka minne na nusu hakuwahi kumaliza na mabao 10 kwenye ligi namba zake zilikuwa za kawaida sana ambapo msimu wake wa kwanza 2021/22 ndio alifunga sana akimaliza na mabao nane.

Msimu uliofuata 2022/23 namba zikaanza kupungua badala ya kupanda akimaliza na mabao mawili pekee wakati msimu wa 2023/24 akashuka zaidi akimaliza na bao lake moja, ukafuata msimu wa 2024/25 yaani msimu uliopita akafunga mabao manne tu na msimu huu mpaka anaondoka kwenye ligi akiwa hana bao lolote.

Aliyekuwa mchezaji wa Simba, Kibu Denis ambaye kwa sasa amejiunga na Al Nasr ya Libya. Picha na ,Mtandao

Aliwahi kutoroka

Wakati Simba ikijiandaa na kuanza msimu mpya uliopita taarifa iliyoshtua ni kutoroka kwa Kibu akionekana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere bila ruhusa ya klabu yake hali iliyozusha sintofahamu kubwa.

Ilielezwwa kwamba Kibu alikwenda nchini Norway kwa majaribio lakini hakuwa amepata ruhusa ya klabu yake, hata hivyo dili hilo likakwama na akarejea nchini, akikosa maandalizi ya mwanzo ya msimu na timu yake.

Itakumbukwa Msemaji wa Simba Ahmed Ally wakati wa tamasha la Siimba day alilazimika kumwombea msamaha kiungo huyo mshambuliaji kwa mashabiki wa timu hiyo ambao nao waliamua kumsamehe na maisha yakaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *