Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeanza utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan akiitka mamlaka hayo kuongeza wigo wa utoaji huduma.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda akiwa ziarani Karatu amesema, wakati wa kampeni za uchaguzi 2025 Rais Samia aliahidi kuongeza wigo wa huduma za kodi ndani ya siku 100 na kuwa hatua za utekelezaji zimeanza.
Kamishna Mwenda amesema tayari amekutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara mbalimbali wakiwamo waendeshaji wa shughuli za utalii kabla ya kufanya maamuzi ya aidha kuanzisha mkoa wa kodi au kupanua huduma.
Katika ziara hiyo Kamishna Mwenda amekutana pia na Mkuu wa Wilaya ya Karatu Dkt, Lameck Karanga ambako amewahakikishia walipakodi wote kuwa wataendelea kuwezesha biashara zao na kuwapa huduma bora kwa kutumia mifumo ya kidijitali ikiwamo IDRAS.
Naye Dkt Karanga amesema wamefurahishwa na ujio wa Kamishna Mkuu kwenye eneo lao na kuwa wilaya anayoiongoza ina uchumi mkubwa ambao unaotokana na shughuli za utalii.
Akiwa Karatu Kamishna Mkuu Mwenda amewatembelea baadhi ya Walipakodi akiwamo Gibbs Farm ambapo msimamizi wa fedha, George Seostine amemshukuru Kamishna Mkuu kwa kuwatembelea na kuwasikiliza na kuipongeza TRA kwa kuanzisha mfumo wa IDRAS ambao utakuwa tiba ya changamoto za Kodi.

(Feed generated with FetchRSS)