
Palestina imekaribisha matokeo ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, ambao umesisitiza tena upinzani wa bara hilo dhidi ya mipango ya kuwafukuza Wapalestina katika nchi yao na kuunga mkono suala la Palestina kupata uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa.
Hayo yamekuja katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina kufuatia taarifa ya mwisho ya Mkutano wa 39 wa Afrika, uliofanyika Februari 14 na 15 katika mji mkuu wa Ethiopia, ukihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres. Mkutano huo ulijadili masuala ya usalama na hali ya hewa, na kujaribu kuzuia migogoro ya ndani katika nchi bara hilo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imepongezi misimamo iliyo wazi na thabiti iliyosisitizwa katika mkutano huo, ikisema inaakisi uungaji mkono wa bara la Afrika kwa haki zisizopingika za watu wa Palestina.
Taarifa hiyo pia imepongeza wito wa mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika wa kukomeshwa uvamizi wa Israel na kuharakishwa mchakato wa kuipa nchi ya Palestina uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa, ikisisitiza kuwa hiyo ni haki ya kisiasa na kisheria.
Katika taarifa yake ya mwisho, Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika umesisitiza tena upinzani wake dhidi ya jaribio lolote la kuwahamisha watu wa Palestina kwa nguvu na kuwapeleka Misri au Jordan, ikitaja jambo hilo kuwa ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.
Mkutano wa kilele wa Afrika pia umeonya kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza kutokana na vikwazo vya Israel, ukieleza mshikamano wake kamili na mapambano ya kupigania uhuru ya Wapalestina na kuanzisha taifa lao huru kwenye mipaka ya 1967.