Dar es Salaam. Tarehe ya leo, Februari 16,2026 unatimia mwaka mmoja rasmi tangu mwanamitindo Hamisa Mobetto kufunga ndoa na nyota wa zamani wa Yanga, Stephanie Aziz KI, MVP wa Ligi Kuu Bara 2023-2024.

Mastaa hao wenye nguvu kubwa ya ushawishi hasa katika mitandao ya kijamii, walifunga ndoa yao kwenye msikiti maarufu wa ‘Masjid Nnuur’ uliopo Mbweni, Dar es Salaam ikiwa ni siku moja baada ya kutolewa kwa mahari.

Hamisa, Miss XXL After School Bash 2010, alilipiwa mahari ya ng’ombe 30 na fedha kiasi cha Sh30 milioni ambapo Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said ndiye alikabidhi kwa niaba ya familia ya bwana harusi.

Tetesi za uhusiano wao zilianza Mei 2024 baada ya kuonekana wakitoka wote Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) pamoja na wachezaji wengine wa Yanga.

Akisherehekea kutimiza umri wa miaka 30 hapo Desemba 10, 2024, Hamisa alichapisha picha yake Instagram ikiwa imepambwa na kalenda, ndipo akathibitisha yeye na Aziz Ki tayari ni wachumba.

Hiyo ni baada ya Aziz Ki kutoa ujumbe kwa lugha ya Kifaransa katika picha hiyo ya Hamisa akisema; “Maisha yenye furaha, kuwa na furaha milele na nuru, heri ya kuzaliwa mchumba. Kisha akamalizia na emoj ya busu!”

Hamisa aliyezaliwa mwaka 1994, huko Mwanza akiwa mtoto pekee kwa mama, hakuwa nyuma kuujibu ujumbe huo, naye alitumia lugha ya Kifaransa akiandika; Merci mon fiancé – akimaanisha, asante mchumba wangu.

Wakati wakiadhimisha mwaka mmoja wa ndoa hiyo, kuna mengi yametokea, ni mchanganyiko wa baraka na changamoto ambazo ni za kawaida katika maisha ya kila siku.

Aprili 2025, yaani miezi miwili baada ya kufunga ndoa, Hamisa na Aziz Ki waliibuka washindi katika tuzo za East Africa Arts & Entertainment Awards (EAEA) zilizotolewa Kenya.

Hamisa alishinda kipengele cha Mwanamitindo Bora Maarufu (Best Fashion Icon Celebrity), huku Aziz Ki akishinda kama Mwanamichezo Bora (Best Sport Personality).

“Asanteni mashabiki wetu kwa kupiga kura, na kila mmoja aliyechangia kwa njia yoyote mafanikio ya chapa zetu. Mbarikiwe sana,” alisema Hamisa kupitia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 10.

Tuzo za EAEA ni kwa ajili ya kuwatunza wasanii, na hata wanamichezo na wabunifu wa mitindo wanaofanya vizuri katika mataifa ya Burundi, DR Congo, Kenya, Rwanda, Tanzania, Uganda na Sudan Kusini.

Ikumbukwe kuna mastaa wengi Bongo tayari wameshinda tuzo hizo ila Rayvanny, mwanzilishi wa Next Level Music (NLM), ndiye amefanya vizuri zaidi akishinda tuzo tano kwa mpigo akifanya hivyo msimu wa 2024.

Mei 2025, yaani miezi mitatu baada ya kufunga ndoa, Aziz Ki alianga rasmi ndani ya Yanga akiwashukuru mashakibiki na viongozi, na kubwa zaidi akiishukuru timu hiyo kwa kumpatia mke mzuri.

“Hii ni zaidi ya kuacha tu klabu, ninaaga nyumba, familia, na sehemu ambayo ilitengeneza mtu na mchezaji niliye leo. Yanga walinipa kusudi. Yanga walinipa nyumba ya pili, na hata kunipa mke mzuri!,” alieleza Aziz Ki katika taarifa yake.

Aziz Ki aliyejiunga na Yanga hapo Julai 2022 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, alifanya vizuri na klabu hiyo ambapo msimu wa 2023/24 alishinda tuzo tatu ikiwemo ya Mchezaji Bora Ligi Kuu (MVP).

Kutokana na kushinda tuzo ya MVP, Aziz Ki alipewa zawadi ya kwenda kupumzika Dubai siku tano pamoja na mwenza wake. Baada ya safari hiyo Hamisa alisema; Yeye [Aziz Ki] ndiye hasa shairi ninalotaka kuandika.

Julai 2025, yaani miezi minne baada ya kufunga ndoa, Hamisa alikuwepo Marekani kumuunga mkono mumewe Aziz Ki katika michuano mipya ya FIFA ya Kombe la Dunia la Klabu akiwa na klabu yake mpya, Wydad AC.

Hatua hiyo likuja takribani mwezi mmoja tangu Aziz Ki kujiunga na miamba hiyo ya Morocco ambapo pia Hamisa aliongozana naye siku aliyoenda kusaini mkataba ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kuondoa Yanga.

Huu ulikuwa ukurasa mpya wenye sura mbili katika ndoa yao, mosi, ni Aziz Ki kupata fursa ya kusajiliwa na moja ya klabu kubwa barani Afrika, hivyo hiyo ilikuwa ni ishara ya baraka za mapema kabisa katika ndoa.

Pili, umbali kati yao, Aziz Ki akihamia Casablanca, Morocco, huku Hamisa akiendelea kuishi Dar es Salaam, kwa ndoa kama yao lazima kuwe na changamoto za hapa na pale ukizingatia wote bado vijana halafu maarufu, hivyo vishawishi vinaweza kuwa vingi.

Hata hivyo, mara kadhaa walikuwa wakitembeleana, hata sasa ambapo Aziz Ki amejiunga na Al Ittihad ya Libya amekuwa akifanya hivyo, mathalani hivi karibuni alikuwa Dar es Salaam ambapo yeye na mkewe Hamisa walihudhuria show ya Davido kutoka Nigeria pale Lugalo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *