Dar es Salaam. Kila mwaka ifikapo Machi 8, huadhimishwa Siku ya Wanawake Duniani, ikilenga zaidi kutambua uwezo wa wanawake katika nyanja tofauti kwa jamii zinazowazunguka, kitaifa na kimataifa.
Kuonyesha kuthamini hilo, Mwananchi linachambua wanawake mbalimbali wenye ushawishi mkubwa katika michezo na burudani na wamekuwa mfano wa kuigwa katika kujituma kwao na kujitengenezea kipato.
Miongoni mwa wanawake hao yupo msanii maarufu wa filamu, Queenie Oscar Masanja, ambaye ni mjasiriamali, mwigizaji na balozi ya bidhaa mbalimbali.
Kipaji chake kimekuwa na mvuto mkubwa kwa mashabiki wanaofuatilia. Kwa mara ya kwanza alianza kuonekana katika tamthilia ya Kaza Moyo iliyolenga zaidi kuonyesha maisha ya watu wa uswahilini.
Mwanadada huyo mrembo, uhusika wake katika tamthilia hiyo alikuwa ni mwanamke asiye na upendo, jambo ambalo alisema ni tofauti na uhalisia wa maisha yake.
Kabla ya kuanza kuigiza aliteka mitandao ya kijamii iliyomzungumzia kutokana na sakata la kudai talaka kwa aliyekuwa mume wake, Dk Mwaka aliyejaaliwa kupata naye watoto wawili.
Wakati anadai talaka mara nyingi alionekana ni mwanamke mwenye huzuni. Lakini baada ya kufanikiwa upepo ulibadilika na muda mwingi anaonekana mwenye tabasamu na mchapakazi.
Kwa sasa anaigiza katika tamthilia ya Jua Kali kama bosi ofisini na mke wa Patrick ambaye ni Zembwela na anachepuka na Enzo rafiki wa mdogo wake Davis.
Kwa jinsi anavyoupatia uhusika, wengi wao wanaona kama maisha ya kweli kwa namna wanavyotuma maoni yao katika mitandao ya kijamii na wengi wakienda mbali kumuona alitaka uhuru wa kuachana na mume wake ili afanye hayo.
Katika tamthilia hiyo anajulikana kwa jina la Regina, mchapakazi, lakini anayesumbuliwa na mapenzi, licha ya mume wake wa maigizo Patrick kumpenda sana.
TUZO YA USHAWISHI AFRIKA
Queenie ni mwanamke mwenye ushawishi mkubwa katika mitandao ya kijamii na alipata tuzo ya Best Influencer Afrika 2025 na alipozungumza na Wanahabari alisema: “Hiyo ni tuzo yangu ya saba, inanipa moyo wa kuendelea kupambana, kwani nimekutana na changamoto ya kukatishwa tamaa, lakini sikurudi nyuma.”
“Nawashauri wanawake wenzangu wasiache kupambana na shughuli mbalimbali iwe wanauza mboga, mama lishe, wanashona nguo ili mradi wanaweza wakajipatia kipato cha kujikimu kimaisha wasikubali kukata tamaa,” aliongeza mwanadada huyo.
Kutokana na urembo alionao, Queenie amekuwa akipata dili mbalimbali za kuwatangazia watu nguo kwa kuvaa, wakati mwingine anazishikilia na kuzitembeza mtaani. Ukiacha hilo anatangaza bidhaa mbalimbali kama maua, kuuza magari, runinga, jambo linalomuonyesha ni mwanamke jasiri, mpambanaji aliyeamua kusimama kwa miguu yake mwenyewe.
“Nilianza harakati za matangazo kuanzia mwaka 2006 katika kampuni mbalimbali za wanamitindo, baadaye nikawa kimya. Ninachokifanya kwa sasa ni kile nilichojifunza nyuma, kipindi hiki nafanya kwa ubora, maneno ya watu hayazuiliki. Mimi ni mwanamke niliye na majukumu, sifanyi ili nionekana najaribu kufanya kilichopo ndani ya uwezo wangu,” anasema Queenie.
KAUZA SURA VIDEO YA NANDY
Katika video ya wimbo wa Asante wa mwimbaji wa Bongo fleva, Faustina Charles Mfinanga almaarufu kama Nandy, ambayo amewashirikisha watu mbalimbali, Queen ni miongoni mwao na anaonekana kufanya vizuri kwa upande huo. Jambo linalozidi kumjengea heshima na kufanyika mfano wa kuigwa kwa mabinti kujituma katika vitu wanavyovifanya.
Mbali na uigizaji na kufanya matangazo ya biashara za wengine, Queen anamiliki Shule ya awali ya watoto wadogo (Day care) inayojulikana kwa jina la Parkland iliyopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam inayopokea watoto kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi mitano, jambo ambalo alipongezwa na watu wengi ikiwemo baadhi ya mastaa wenzake.