RAIS Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuweka historia mpya barani Afrika kwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza mwanamke wa Umoja wa Afrika (AU) ifikapo mwaka 2028. Endapo hatua hiyo itakamilika, atakuwa kiongozi wa tatu kutoka Tanzania kushika wadhifa huo wa juu katika umoja huo wa bara la Afrika, hatua inayoendelea kuiweka nchi katika nafasi ya kipekee kidiplomasia na kiuongozi.
Akizungumza na wanahabari Ikulu jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, amesema matarajio hayo yanaakisi imani kubwa ya mataifa ya Afrika kwa uongozi wa Rais Samia pamoja na mchango wa Tanzania katika masuala ya amani, usalama na maendeleo ya bara hilo. SOMA: Rais Samia ajizatiti malengo Dira 2050
Amesisitiza kuwa historia ya Tanzania katika medani za kimataifa imejengwa juu ya diplomasia thabiti, mshikamano wa kikanda na ushirikiano wa kimkakati. Tanzania imewahi kushika nafasi hiyo kupitia Baba wa Taifa, Julius Nyerere mwaka 1978 na baadaye Jakaya Kikwete mwaka 2008. SOMA:

Katika mkutano huo uliofanyika Februari 16 na kuratibiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, viongozi mbalimbali pia wameelezea mafanikio ya ziara mbili za kikazi za Rais Samia nje ya nchi. Kuanzia Februari 3–6, Rais alishiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi Duniani uliofanyika katika Falme za Kiarabu (UAE) ambako aliwasilisha ajenda za uwekezaji, ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo endelevu.
Baadaye, Februari 12–15 alihudhuria Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia, ambapo masuala ya amani, usalama na maendeleo ya Afrika yalijadiliwa kwa kina. Waziri Kombo amesema Tanzania inatarajiwa kushika nafasi ya Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) ifikapo mwaka 2029, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha sauti ya nchi katika masuala ya amani na usalama wa kimataifa.
Amebainisha kuwa Tanzania tayari imehudumu kama Mjumbe wa Baraza la Usalama la AU kuanzia mwaka 2022 hadi 2026, ikichangia katika maamuzi muhimu ya utatuzi wa migogoro na ulinzi wa raia barani Afrika, uzoefu unaotajwa kuwa msingi imara kuelekea safari ya UN mwaka 2029.