Wakati mivutano kati ya Iran na Marekani inazidi kuongezeka, Tehran imesisitiza kuwa, machaguo yake yote yako mezani, licha ya mazungumzo yanayoendelea baina yake na Washington.

Kwa mujibu wa Pars Today, sambamba na kushtadi mivutano kati ya Iran na Marekani na kuongezeka kiwango cha vitisho vya kijeshi vinavyotolewa na Washington, Tehran imesisitiza kuwa, licha ya kuendelea mazungumzo, machaguo yote yako mezani, kuanzia utumiaji wa makombora yake hadi ufungaji wa Lango-Bahari la Hormuz.

Mnamo Februari Mosi, Meja Jenerali Sayyid Abdolrahim Mousavi, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Iran, aliashiria vitisho vinavyotolewa na adui na akasema: “kosa dogo kabisa litafungua mikono yetu kwa ajili ya kuchukua hatua, na dunia itashuhudia sura tofauti ya Iran imara yenye nguvu; na wakati huo, hakuna Mmarekani atakayebaki salama, na moto wa eneo hili utaiteketeza Marekani na washirika wake”.

Leo Jumatatu, Februari 16, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araghchi, amegusia safari yake ya mjini Geneva na kusema, anaelekea huko akiwa na mipango halisi ya kufikia makubaliano ya haki na usawa, na akasisitiza kwamba: “kile ambacho hakiko kabisa katika ajenda ni kusalimu amri mbele ya vitisho.”

Sayyid Abbas Araghchi

Msimamo wa Iran wa kuendeleza mazungumzo na wakati huo huo kuweka mezani machaguo yote unaweza kutafsiriwa kama uchanganyaji wa hatua ya kuzuia hujuma ya kijeshi, kujijengea wenzo wa kijiopolitiki, na kuwa na udhibiti wa anga ya kidiplomasia. Maelezo hayo, kwa hakika ni ufikishaji ujumbe wenye matabaka kadhaa kwa wadau tofauti: kwa wananchi wa Iran ni kujenga mshikamano wa ndani, kwa Marekani ni kutathmini utashi wake na gharama zitakazoikabili, na kwa wadau wa kikanda na soko la nishati, ni kuwakumbusha unyeti na uhasasi wa milingano ya masuala mbalimbali katika Ghuba ya Uajemi.

Tabaka la kwanza ni uzuiaji hujuma za kijeshi. Linapoashiriwa “kombora” katika misamiati rasmi ya kijeshi inamaanisha kutilia mkazo uwezo wa ndani ya nchi katika sekta za makombora na ndege zisizo na rubani ambazo kwa miaka kadhaa sasa zimekuwa zikifafanuliwa kama nguzo na mihimili mikuu ya doktrini ya ulinzi ya Iran. Japokuwa uwezo huu una ufanisi wa kijeshi wa kushangaza, lakini kazi yake ya msingi ni kuufanya upande wa pili usijipe uhakika wa ushindi na kuutanabahisha juu gharama kubwa utakayolipa kwa hatua yoyote ya moja kwa moja ya kijeshi utakayochukua. Katika mfumo wa doktrini ya kumzuia adui asishambulie, kuonyesha uwezo wa kujibu mapigo kwa haraka na ya ngazi kadhaa kunaweza kubadilisha mahesabu ya adui na kuielekeza anga ya hali ya mambo kwenye hatua ya kudhibiti mgogoro. Katika vita vya siku 12 ulivyoanzisha utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, Tehran ilionyesha kwamba makombora yake kadhaa ya “Fat-h” na “Khaybar-shekan” yana uwezo wa kuangamiza vituo vya utafiti wa kijeshi vya Israel, viwanda vyake vya kusafisha mafuta, na miundombinu yake ya kiuchumi.

Hii ni pamoja na kwamba, hivi karibuni, Meja Jenerali Mousavi alieleza katika taarifa aliyotoa kuhusu mabadiliko iliyofanyiwa doktrini ya kijeshi ya Iran ya kwamba: “Baada ya vita vya siku 12 na kuendelea hatua za kimaudhi za Kimarekani na Kizayuni, tuliangalia upya doktrini ya ulinzi ya nchi na kuibadilisha kuwa doktrini ya ushambuliaji ya vikosi vya ulinzi, inayotumia mbinu ya utekelezaji operesheni za kasi kubwa mno na zinazoenea kwenye mduara mpana, kwa kutekeleza mikakati ya kijeshi isiyo na mlingano na ya vipigo vikali. Kwa hiyo, hatua yetu itakuwa ya kasi, kali, na isiyotarajiwa katika mahesabu ya Marekani.”

Tabaka la pili ni la wenzo wa kijiopolitiki, ambao unafahamika kwa uwazi zaidi kwa kutajwa Lango-Bahari la Hormuz. Kivuko hicho ni moja ya mikondo muhimu zaidi ya kupitishia nishati duniani, na tishio lolote dhidi ya usalama wake huwa na athari za ghafla kwa soko la mafuta, bima ya vyombo vya majini, na usalama wa usambazaji wa mafuta kimataifa. Kuashiria nukta hiyo nyeti na hasasi, badala ya kuonyesha nia ya kuchukua hatua kivitendo, kunafanyika zaidi kama turufu ya kutumiwa katika majadiliano na kukumbusha juu ya kuwepo “uwezo wa kuathiri mambo kwa njia isiyo ya moja kwa moja”. Katika mazingira ambapo usalama wa nishati unategemea sana utulivu wa Ghuba ya Uajemi, hata ongezeko la hisia ya hatari tu linaweza kupangua bei na kuongeza mashinikizo ya kisiasa katika ngazi ya kimataifa.

Kwa muktadha huo, ikiwa hali itakuwa ngumu kwa Iran, kuna chaguo kwamba, njia za mabadilishano ya kibiashara na upitishaji bidhaa kwa nchi zingine duniani, zitakuwa ngumu pia, na hilo linawezekana kwa kulifunga Lango-Bahari la Hormuz. Kutokana na Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na makombora ya kutokea pwani kuelekea baharini vitaweza kulitekeleza hilo kwa mbinu tatu za “makombora ya kuripua meli, mabomu ya kutegwa majini, na vyombo vya doria”.

Na tabaka la tatu ni udhibiti wa medani ya kijeshi na diplomasia kwa wakati mmoja. Sisitizo la kuendeleza mazungumzo sambamba na kubainisha uwepo wa machaguo magumu ni kufanya juhudi za kudumisha njia za mawasiliano pasi na kuacha nyenzo za kijeshi. Mbinu hii inaonyesha kwamba, Tehran inajitahidi, kwa upande mmoja kuweka wazi mlango wa mazungumzo ili kuzuia kushtadi mivutano; na kwa upande mwingine, kuimarisha turufu yake ya majadiliano kwa kuyapa uzito mkubwa machaguo yenye gharama kubwa. Katika hali kama hii, lugha ya vitisho huwa si lazima iwe ni ishara ya kupendelea makabiliano, lakini inachukuliwa kuwa ni sehemu ya “lugha ya nguvu” katika mazungumzo magumu.

Kwa ujumla ni kwamba, msimamo wa Iran unaweza kutafsiriwa kama juhudi za kutengeza “mwavuli wenye pande kadhaa za kuzuia hujuma” huku ukiweka wazi mlango wa diplomasia. Ujumbe mkuu ni ni kwamba: Mazungumzo huwa na maana, pale pande zote zinapoihisi gharama ya kuvunjika kwake. Na wakati huo huo, msimamo wa Tehran unabeba ujumbe kuwa, Iran imejiweka tayari kikamilifu kutoa jibu kwa sinario zote zinazoweza kusababishwa na maadui zake, hususan Marekani na utawala wa Kizayuni…/

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *