KAMATI ya Bunge ya Miundo Mbinu imeishauri Serikali kuwaingiza kwenye mfumo wa mikopo wanafunzi wa urubani katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), ili kupunguza changamoto ya ada kubwa na kuwawezesha kumaliza masomo bila vikwazo vya kifedha.
Akizungumza Februari 16, 2026 kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Johnston Mutasingwa amesema baadhi ya kozi, hususan urubani, zinagharama kubwa, hivyo kuna umuhimu wa kuwajumuisha wanafunzi hao kwenye mpango wa mikopo ya elimu ya juu. “Tumeshuhudia kuwa gharama za baadhi ya kozi ni kubwa, hivyo kuna umuhimu wa Serikali kuingiza wanafunzi hawa kwenye mfumo wa mikopo ili kuwaondolea mzigo wa ada,” alisema.
Mutasingwa ameongeza kuwa mikopo hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wa taaluma zenye gharama kubwa, huku akisisitiza lengo la kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeishia masomo kwa ukosefu wa ada. SOMA: Rubani aing’arisha Tanzania ndani ya MUFASA

Mbali na suala la mikopo, Kamati hiyo imeishauri Serikali kupitia NIT kununua ndege mbili za mafunzo kwa ajili ya wanafunzi wa urubani, hatua inayolenga kuongeza vitendea kazi na kuboresha ubora wa mafunzo ya anga.
Mkuu wa NIT, Prosper Mgaya amesema mahitaji ya wataalamu wa usafiri wa anga ni makubwa huku akibainisha kuwa kwa sasa kuna upungufu wa wataalamu wa anga unaofikia asilimia 50. “Uwekezaji katika mafunzo ni lazima ili kukabiliana na upungufu huo,” alisema. Mgaya ameongeza kuwa chuo kina mpango wa kununua ndege mbili za mafunzo kwa wanafunzi wa urubani ili kuendana na kasi ya masomo na mahitaji halisi ya sekta ya anga.