Vikosi vya Israel vimewaua angalau Wapalestina 10 katika mashambulizi mapya yaliyofanywa katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza, katika ukiukaji mwingine wa makubaliano ya usitishaji vita yaliyoratibiwa na Marekani na kuanza kutekelezwa Oktoba 10 mwaka jana.

Chanzo cha kitabibu katika Hospitali ya Nasser Hospital kimesema watu wanne waliuawa Jumapili katika shambulizi la Israel katika mji wa kusini wa Khan Younis.

Imedokezwa  kuwa magari ya wagonjwa hayakuweza kufika katika eneo hilo kutokana na kizuizi kilichowekwa na ndege zisizo na rubani za Israel zilizokuwa zikiruka juu ya eneo la jinai.

Wapalestina wengine wanne waliuawa baada ya vikosi vya Israel kushambulia hema la wakimbizi katika eneo la al-Faluja, kaskazini mwa Gaza.

Taarifa kutoka hospitali za Gaza pia zinaonyesha kuwa Wapalestina wawili wengine waliuawa katika mashambulizi hayo ya Israel, ingawa eneo husika na utambulisho wa waathirika haukutajwa mara moja.

Kwa mujibu wa mamlaka za Gaza, Israel imekiuka makubaliano ya usitishaji vita zaidi ya mara 1,500 tangu yalipoanza kutekelezwa Oktoba mwaka jana. Tangu wakati huo, watu wasiopungua 591 wameuawa na 1,590 kujeruhiwa.

Makubaliano hayo yalimaliza mauaji ya kimbari ambayo yalianza kutekelezwa na jeshi la Israel dhidi ya Wapalestina mnamo Oktoba 8, 2023 na kudumu kwa takribani miaka miwili.

Kwa mujibu wa maafisa wa Palestina, vita hivyo vilisababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 72,000 na kujeruhi zaidi ya 171,000, wengi wakiwa ni wanawake na watoto, huku takribani asilimia 90 ya miundombinu ya kiraia ikiharibiwa kwa kiwango kikubwa.

Umoja wa Mataifa umekadiria kuwa gharama za ujenzi upya wa Gaza zitafikia takribani dola bilioni 70 za Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *