ZAIDI ya Wasichana 13,000 wenye umri kati ya miaka 13 na 21 waliokatisha masomo ya sekondari kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ujauzito, wamejisajili na kurudi shuleni kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari kwa Njia Mbadala (SEQUIP-AEP) ulioanza mwaka 2022 na kufikia mwaka 2026.

Akifungua kikao kazi Mkoani Morogoro kilichowashirikisha watekelezaji wa mikoa 26 ya Tanzania Bara,Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Profesa Philipo Sanga amesema mradi huo umetekelezwa na TEWW chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TEMISEMI) na ufadhili wa Benki ya Dunia.

“Jukumu letu ni kuwarejesha shuleni watoto waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali zikiwemo mimba za utotoni, ajira za watoto, kuolewa kabla ya wakati na hali za kiuchumi za familia zao. Mradi ulianza mwaka 2022 na mwaka huu ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji,” alisema Profesa Sanga. SOMA: Wanafunzi wa kike kuunganishwa vyuo vya ufundi

Profesa Sanga amesema kwa kipindi hicho walikuwa na jukumu la kurejesha watoto 12,000, lakini hadi sasa wamefanikisha kurejesha zaidi ya 13,000, sawa na asilimia 100 ya lengo lililotolewa na Serikali. “Watoto hawa wanaendelea kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita, vyuo vya kati na vyuo vikuu.

Wakati mwingine tunapaswa kufikiria jinsi Taasisi itaendelea na jukumu hili kwa njia nyingine ili kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nyuma,” aliongeza. Mradi huo pia umewezesha uboreshaji wa miundombinu ya masomo kwa kujenga majengo ya madarasa, hosteli na maktaba mikoani.

Hata hivyo, Profesa Sanga amesema changamoto bado zipo, kwani baadhi ya wazazi na walezi hawakukubali watoto wao kurejea shuleni mara nyingine. Kwa upande wao, wakufunzi kutoka TEWW wamesema mradi huo umewapa manufaa makubwa watoto wa kike na wa kiume waliokatisha masomo, na kurejea tena shuleni kwa mfumo usiorasmi kunawasaidia kufanikisha masomo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *