WATU watano wamefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi katika machimbo ya mchanga ya Bolbit, Kijiji cha Makuyuni, Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amesema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11:30 jioni tarehe 16 Februari 2026, kufuatia kuporomoka kwa kingo za udongo (ngema) na kuwaangukia waliokuwa wakichimba mchanga.
Jitihada za uokoaji zilihusisha Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wananchi, na kufanikiwa kutoa miili ya marehemu wote watano. Miili hiyo imehifadhiwa Hospitali ya Halmashauri ya Korogwe Vijijini, Makuyuni, kwa taratibu zote. SOMA: Polisi yamsaka mwanamke aliyeiba mtoto wa siku moja
Waliopoteza maisha ni Shabani Mrisho maarufu Mwantembo (31), Yusuph Abdalah maarufu Kibaya, Juma Hatibu maarufu Msikiti (49), Nurdini Amiri maarufu Daffa (30), na Zamiru Miraji maarufu Daffa (35). Wote walikuwa wakazi wa Makuyuni na wakijihusisha na kilimo, huku baadhi yao pia wakijihusisha na uchimbaji.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi wanaojihusisha na uchimbaji kuzingatia kanuni na misingi ya usalama ili kuepuka ajali zinazoweza kusababisha vifo na maafa kwa familia na jamii. Viongozi wa vijiji na mitaa wametakiwa kusimamia kwa karibu shughuli za machimbo ili kuhakikisha zinafanyika katika mazingira salama.
