WAZIRI Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza wajumbe wa kamati mapokezi na kamati za ujenzi za mradi wa ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza wakamatwe mara moja na kuhojiwa kuhusu upotevu wa vifaa vya mradi huo.

“Kunadon 700, Marine boards 500 na matofali 2,000 havijulikani viko wapi. Wahusika mnaripoti kazini kila siku na mishahara mnalipwa, lakini ujenzi umesimama,” amesema wakati akimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dkt. Jumaa Mhina. SOMA: Mwigulu akerwa ukosefu matundu ya vyoo shuleni

Agizo hilo alilitoa leo (Jumatatu, Februari 16, 2026) wakati akizungumza na wananchi wa Lusanga, kata ya Mgomeni, wilayani Muheza, waliohudhuria uwekaji wa jiwe la msingi la ofisi hiyo itakayokuwa na ghorofa moja. “Kamanda wa TAKUKURU, ninahitaji taarifa hii kwa kina kabla sijamaliza ziara yangu mkoani Tanga. Kila mmoja ahojiwe ili tujue vifaa vilipoteaje,” alisisitiza.

Dkt. Nchemba ameeleza kuwa baadhi ya vifaa vilinunuliwa lakini vimekaa stoo bila kuanza hatua za ujenzi. “Mshauri mwelekezi wa mradi yupo lakini hamsikilizi ushauri anaotoa,” alisema. Kaimu Mkuu wa Idara ya Miundombinu na Maendeleo Mijini na Vijijini, Mhandisi Abdalla Jaha, alisema mradi huo umefikia asilimia 68 na kuanza Septemba 29, 2023. Wanatarajia ifikapo mwishoni mwa Juni 2026 sakafu ya chini ianze kutumika.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amempongeza kiwanda cha vifungashio cha Yogi PolyPack kilichopo Pongwe, Manispaa ya Tanga, kwa uwekezaji mkubwa na matumizi ya teknolojia ya kisasa. “Unatengeneza ajira, unazalisha bidhaa na unachangia kipato kwa wafanyakazi. Haya ndiyo mambo Rais anataka kuyaona,” alisema.

Pia alitembelea bandari ya Tanga, kukagua uboreshaji wa gati mbili mpya na shughuli za bandari. Waziri Mkuu ameahidi Serikali itaendelea kushughulikia changamoto za kiutumishi na uhaba wa vifaa vya kupakulia mizigo. “Tunatambua ushindani wa kibiashara, lakini tutaendelea kufanya maboresho ili kunufaika na nafasi ya kijiografia ya mkoa wetu,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *