WAZIRI MKUU ANUSA WIZI MWINGINE MUHEZA, AAGIZA KAMATI YA UJENZI WAKAMATWE
Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba ameagiza wajumbe wa Kamati mapokezi na Kamati za Ujenzi za mradi wa ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza wakamatwe na kuhojiwa mara moja ili watoe taarifa juu ya upotevu wa vifaa vya mradi huo.
“Kuna nondo 700, Marine boards 500 na matofali 2,000… hivi vifaa havijulikani viko wapi. Wahusika kila siku mnaripoti kazini, na mishahara mnalipwa wakati ujenzi umesimama na hakuna hatua zinazochukuliwa,” amesema wakati akimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dkt Jumaa Mhina.
Ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na wananchi wa Lusanga, kata ya Mgomeni, wilayani Muheza waliofika kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la ofisi hiyo itakayokuwa na ghorofa moja pindi ikikamilika.
“Kamanda wa TAKUKURU ninahitaji hii taarifa kwa kina kabla sijamaliza ziara yangu mkoani Tanga. OCD fuatilieni kwa kina ushiriki wa watumishi wa hii Halmashauri. Kila mmoja ahojiwe hadi tujue vifaa vilipoteaje.”
Amesema anazo taarifa kwamba timu ya manunuzi imenunua vifaa ambavyo vimewekwa stoo wakati hatua yake ya ujenzi haijafikiwa. “Nimeambiwa vifaa vingine vimekuja lakini vimekaa stoo tu. Ni kwa nini mmenunua wakati hamjamaliza hatua ya kwanza Mshauri mwelekezi wa mradi yupo lakini hamsikilizi ushauri anaotoa,” alisema.
Jengo hilo ndiyo limemalizika kujengwa ghorofa ya chini na linasubiri kuanza kuwekewa linta kwenye ghorofa ya kwanza.
Waziri Mkuu amekemea tabia ya kutochukua hatua masuala kama hayo yanapojitokeza hasa ikizingatiwa kwamba Halmashauri nyingine ambazo walipewa fedha kwa wakati mmoja wao wameshakamilisha kazi ya ujenzi.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Miundombinu na Maendeleo Mijini na Vijijini, Mhandisi Abdalla Jaha alisema mradi huo ambao umefikia asilimia 68, ulianza kujengwa Septemba 29, 2023 na wanatarajia ifikapo mwishoni mwa Juni, 2026 sakafu ya chini ianze kutumika.
(Feed generated with FetchRSS)