1. Mkutano wa AI waanza New Delhi Mjumbe wa UN asisitiza ujumuishi wa nchi zote

Mkutano wa kimataifa unaofahamika kama AI Impact 2026 umeanza leo mjini New Delhi, India ukiwakutanisha viongozi kutoka sehemu mbalimbali za dunia ili kujadili namna akili mnemba (AI) inavyoweza kuendelezwa na kutumika kwa uwajibikaji kuchangia maendeleo endelevu. Amandeep Singh Gill, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia teknolojia za kidijitali na zinazoibuka, amesisitiza ushiriki mpana wa kimataifa kwani ni muhimu ili kuhakikisha AI inanufaisha nchi zote.

Mkutano huo wa siku tano, ulioandaliwa na Wizara ya Teknolojia ya Habari ya India umewaleta pamoja serikali, sekta binafsi, wanazuoni, asasi za kiraia na mashirika ya kimataifa na zaidi ya matukio 30 yaliyoandaliwa na mfumo wa Umoja wa Mataifa yatajadili masuala kuanzia kilimo na uhakika wa chakula hadi usawa wa kijinsia, afya ya umma, kupunguza hatari za majanga na usalama wa watoto mtandaoni.

Akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko India, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia teknolojia za kidijitali na zinazoibuka Amandeep Singh Gill ameuelezea mkutano huo kama hatua muhimu kwa ushiriki wa nchi za Kusini mwa Dunia katika kuunda sera na kanuni za Akili Mnemba, AI. Amesisitiza kuwa ujumuishaji ni muhimu ili kunufaika na fursa na kudhibiti hatari, akitaja mapendekezo ya mfuko wa kimataifa wa kujenga uwezo wa AI wenye thamani ya hadi dola bilioni 3 pamoja na mtandao wa vituo vya mafunzo utakaosaidia nchi kuimarisha ujuzi, rasilimali za data na miundombinu ya kidijitali.

Ameonya kuwa wanawake bado hawajawakilishwa ipasavyo katika utafiti, uwekezaji na uongozi wa AI, ingawa amebainisha mifano inayotia moyo ya wanawake wanaoongoza ubunifu katika maeneo kama tathmini ya usalama, utofauti wa lugha na mifumo huria ya AI.

Deep Aman Gill, kiongozi wa kiteknolojia wa India aliyevaa turban ya bluu na suti, anaongea katika mkutano wa AI Summit USG, akiashiria kwa mikono yake.

Deep Aman Gill akizungumza katika mkutano wa AI Summit USG

Kuhusu hatari kama taarifa potofu, upendeleo na vitisho vya usalama, Gill bila shaka, ni mjadala wenye changamoto kwa sababu uhuru wa kuzungumza, na kiwango ambacho unaweza kudhibiti yaliyomo kwenye majukwaa ya kidijitali ni mada nyeti ambapo nchi zina mitazamo tofauti. Lakini anadhani Umoja wa Mataifa unaweza kucheza jukumu la kuunganisha mitazamo hii tofauti, kuiunganisha na haki msingi za binadamu na na haja ya kulinda demokrasia na haki msingi.

Ameongeza kuwa ingawa AI inaweza kusaidia kufuatilia uzalishaji wa hewa chafuzi na kuboresha matumizi ya nishati, ukuaji wake wa haraka unaongeza mahitaji ya nishati, maji na malighafi. Amesisitiza pia umuhimu wa sera zinazoweka kipaumbele kwa masuala ya tabianchi, bayonuai na mazingira katika maendeleo ya AI.

Akitazama miaka mitano ijayo, Gill amesema mafanikio yatamaanisha nchi nyingi zaidi kuwa na uwezo wa kuendeleza na kusimamia AI kwa kutumia vipaji, data na miundombinu yao wenyewe, huku ushirikiano wa kimataifa ukisaidia kuoanisha viwango na kuepuka mgawanyiko wa kanuni.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye amerejea leo jijini New York, Marekani akitoka jijini Addis Ababa katika mkutano wa Muungano wa Afrika, AU, anatarajiwa kuelekea nchini India kushiriki katika katika mkutano huu wa kimataifa wa AI.

Mkutano huu ni msingi muhimu kuelekea mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu utawala wa Akili Mnemba utakaofanyika mwaka huu mwezi Julai jijini Geneva, Uswisi.

media:entermedia_image:5866a6da-ed67-4cdb-a296-b793674d6e2b

Unsplash/Jennifer Chen

Mandhari ya barabarani huko Havana, Kuba (Maktaba)

2. Cuba: Hali ya kibinadamu imefikia pabaya yaonya OHCHR

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR) imetoa onyo kali kuhusu kuzorota kwa hali ya kiuchumi nchini Cuba, ikisema uhaba wa mafuta na vikwazo vya muda mrefu vinaathiri vibaya huduma za msingi kote nchini humo. 

Akizungumza mjini Geneva Uswis, msemaji wa Ofisi hiyo, Marta Hurtado, amesema hali imefikia pabaya na hakuna dalili ya kutengamaa inaendelea kuzorota

“Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu kuzorota kwa hali ya kijamii na kiuchumi nchini Cuba katikati ya vikwazo vya muda mrefu vya kifedha na kibiashara, majanga ya tabianchi, pamoja na hatua za hivi karibuni za Marekani za kuzuia usafirishaji wa mafuta. Hali hii ina athari kubwa zaidi kwa haki za binadamu za watu wa Cuba.”

Marekani iliweka vikwazo vya kibiashara dhidi ya Cuba mwanzoni mwa miaka ya 1960 kufuatia mapinduzi ya Cuba. Kwa zaidi ya miongo sita, mfumo huo wa vikwazo umepanuka na kujumuisha masharti makali ya kifedha na ya kisekta. Wakati Washington ikisema hatua hizo zinalenga kuhamasisha mageuzi ya kidemokrasia, wakosoaji wanasema zina madhara mapana ya kibinadamu.

Marta Hurtado, Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu

UN /Elma Okic

Marta Hurtado, Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa ofisi ya Umoja wa Mataifa, uhaba wa mafuta wa sasa unaongeza shinikizo katika uchumi ambao tayari uko taabani.

“Kwa kuzingatia utegemezi wa mifumo ya afya, chakula na maji kwa mafuta yanayoagizwa kutoka nje, uhaba wa sasa wa mafuta umeweka upatikanaji wa huduma hizo muhimu hatarini kote nchini”. 

Bi Hurtado ameonya kuwa wodi za wagonjwa mahututi na wodi za huduma za dharura zimeathirika, uhifadhi na usambazaji wa chanjo, damu na dawa nyingine zinazohitaji ubaridi maalum pia viko hatarini kutokana na kukatika kwa umeme kila wakati. Pia upatikanaji wa maji ni changamoto nyingine kubwa inayoongezeka.

“Nchini Cuba, zaidi ya asilimia 80 ya mitambo ya kusukuma maji inategemea umeme, na kukatika kwa umeme kunadhoofisha upatikanaji wa maji salama, huduma za usafi na mazingira. Kukatika kwa umeme pia kunaathiri mawasiliano na upatikanaji wa taarifa.”

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema athari za muda mrefu za vikwazo vya kisekta Cuba zinadhoofisha uwezo wa serikali kutekeleza majukumu yake ya msingi, ikiwemo kutoa ulinzi na huduma kwa wananchi, na zinaweza kuongeza hatari ya misukosuko ya kijamii.

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, amerejea wito wake kwa mataifa yote kuondoa hatua za upande mmoja za kisekta zenye athari kubwa na zisizochagua kwa raia, akisisitiza kuwa malengo ya sera hayawezi kuhalalisha vitendo vinavyokiuka haki za binadamu.

Kwa sasa, ujumbe kutoka Geneva uko wazi, athari za kibinadamu zinaongezeka  na wananchi wa kawaida wa kisiwa cha Cuba ndio wanaolipa gharama kubwa zaidi.

Vyoo vipya katika shule ya msingi ya Lubile iliyoko jimbo la Tanganyika nchini Jamhuri ya Kidemorkrasia ya Congo, DRC. Vyoo hivi vimejengwa kwa msaada wa UNICEF na Education Cannot Wait.

© UNICEF/Josue Mulala

2. UNICEF na KOICA waboresha huduma za usafi na lishe kwa wakazi wa Tanganyika 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF wakishirikiana na Shirika la Maendeleo la Korea KOICA wanawasaidia wananchi wa Nyunzu katika jimbo la Tanganyika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo DRC kwa miradi ya kusaidia huduma za afya ya watoto ambapo wamepanua upatikanaji wa huduma muhimu na endelevu. 

Jimbo la Tanganyika, kijiografia liko kusini mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC, na linapakana na Ziwa Tanganyika, hili ni ziwa refu zaidi la maji safi duniani. Hata hivyo wakazi wa Nyunzu wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji na hii inapelekea wengine kuugua magonjwa yanayosababishwa na uhaba wa maji safi kama vile kipindupindu. 

Jimbo la Tanganyika ni kitovu cha ugonjwa wa Kipindupindu sababu kuu zikiwa uhaba wa maji, wingi wa watu na wakati mwingine mafuriko yanayotokana na kufurika kwa ziwa Tanganyika. 

Wakimbizi wa ndani wakiwa kwenye eneo la kuteka maji lililoandaliwa na UNICEF kwenye viunga vya mji wa Goma,jimboni Kivu Kaskazini, nchini DRC.

© UNICEF/Jospin Benekire

Kwa kutambua changamoto hizo Shirika la UNICEF wakishirikiana na KOICA wanaunganisha nguvu pamoja kuhakikisha wanapunguza magonjwa na vifo miongoni mwa watoto. Na miongoni mwa hatua walizochukua ni pamoja na kuweka vituo vya maji safi ili kuzuia magonjwa yanayosababishwa na maji, mfano, kipindupindu. 

Huyu ni binti mnufaika wa mradi wa maji katika eneo la Nyunzu.

“Tulikuwa tunasafiri kilometa tatu kwenda Katoma kusaka maji, na tukifika huko tunakuta watu wengi hivyo tunangoja mpaka jioni, saa nyingine mnashindwa kupata maji sababu ya ugomvi wa kugombea kupata maji hivyo unaweza kurejea nyumbani bila maji. Nasikia furaha kupata maji kwa sababu KOICA na UNICEF wametuletea maji hapa karibu na nyumbani.” 

Mradi huo pia unafanya uchunguzi iwapo watoto wanaugua utapiamlo. Huyu ni mama mnufaika ambaye baada ya wahudumu wa afya kutembelea anapoishi aligundua mwanaye ni mgonjwa. Akisema “bwakiii” anamanisha utapiamlo. 

“Mimi nilijuwa mwanangu anaugua baada ya kuambiwa na watoa hudumua wa afya wa kijamii, walifika nyumbani wakampima mkono wakagundua anaugua utapiamlo. Watakuelekeza kwenda katika kituo cha afya kwa ajili ya upimaji zaidi ili kugundulika iwapo anaugua utapiamlo. Nikaenda na mwanangu na baada ya kugundulika ni mgonjwa wakampatia dawa ambayo ni chakula cha lishe akaanza kula, na baada ya majuma matatu nikamuona anabadilika na kilo zake zinaongezeka.” 

Huduma nyingine zilizowezeshwa na mradi huo wa UNICEF na KOICA ni pamoja na kuhakikisha kila nyumba ina choo na kila mtu anaelimu stahiki ya kunawa mikono.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *