MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amemaliza mgogoro wa takriban miaka 15 kuhusu umiliki wa nyumba namba 12, kiwanja namba 15, eneo la Kariakoo uliokuwa ukihusisha familia ya marehemu Abdallah Sultani Mtambo na mnunuzi Salim Selemani Salim.

Akizungumza Februari 17 jijini Dar es Salaam baada ya kupokea taarifa ya kamati aliyoiunda, Chalamila amesema amejiridhisha kuwa nyumba hiyo ni mali halali ya Salim Selemani Salim, aliyeinunua mwaka 2011 kwa shilingi milioni 250 kupitia mnada wa mahakama na chini ya usimamizi wa kisheria.

Ameeleza kuwa baada ya mauzo hayo, baadhi ya warithi walipokea fedha zao huku wengine, akiwemo aliyekuwa mke wa marehemu, wakikataa kupokea kiasi cha shilingi milioni 64.5 ambacho bado kipo kwa dalali wa mahakama. Pia ameagiza fedha hizo kuwasilishwa mahakamani ili zikabidhiwe kwa wahusika kwa kufuata taratibu. SOMA: Chalamila arudisha tabasamu kwa Alice

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo na Mwanasheria wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Fabiola Mwingira amesema  uchunguzi umebaini taratibu zote za kimahakama zilifuatwa. Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amepongeza hatua hiyo na kuahidi kushirikiana na vyombo vya usalama kuhakikisha amani inadumishwa katika eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *