DAR ES SALAAM: KUFUATIA ongezeko la matumizi ya huduma za kifedha kupitia mawakala wa mitandao ya simu, Benki ya Equity Tanzania imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na Mixx by Yas kwa lengo la kuimarisha juhudi za kupanua ujumuishi wa huduma za kifedha nchini.

Ushirikiano huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibenki kwa haraka, kwa urahisi na kwa kuaminika katika maeneo mbalimbali bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matawi ya benki.

Uzinduzi wa ushirikiano huo umefanyika lao Februari 17, 2026 jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi wa taasisi hizo mbili pamoja na mawakala wa huduma za kifedha.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Equity Bank Tanzania, Isabela Maganga, amesema lengo la ushirikiano huo ni kuboresha huduma za kibenki kupitia mtandao wa mawakala wa Mixx by Yas ili kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi, ambapo amesema hatua hiyo itapunguza umbali kati ya wateja na huduma za kifedha pamoja na kuwaondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Aidha, ameeleza kuwa ushirikiano huo utawasaidia mawakala kufungua fursa zaidi za kiuchumi kupitia ongezeko la miamala, upanuzi wa wigo wa huduma na kukuza biashara zao. Kwa upande wa jamii, amesema mpango huo utachochea ujumuishaji wa kifedha na kuimarisha mzunguko wa fedha katika uchumi wa ndani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mixx by Yas, Angeliqa Pesha, amesema ushirikiano huo unaakisi mwelekeo wa sekta ya kifedha wa kuunganisha huduma na kuwafikia Watanzania kwa ukaribu zaidi kupitia mawakala wa kampuni hiyo.

“Kwa kuunganisha uzoefu wa kibenki wa Equity na nguvu ya jukwaa la Mixx pamoja na mtandao mpana wa mawakala wetu, tunabadilisha vituo vya huduma vilivyo karibu na jamii kuwa milango kamili ya huduma za kibenki. Kupitia ushirikiano huu, ikiwemo upanuzi wa huduma za utoaji wa fedha za kimataifa (IMT), tunaongeza upatikanaji, urahisi na uaminifu kwa mamilioni ya Watanzania. Kwa pamoja, tunajenga mfumo wa kifedha ulio jumuishi zaidi, unaounganishwa kidijitali na wenye kuwezesha uchumi wa taifa,” amesema Pesha.

Naye mwakilishi wa mawakala, Honest Alfredy, amezishukuru kampuni hizo kwa kuanzisha ushirikiano huo, akisema utasaidia kuongeza fursa mpya za ajira kwa mawakala pamoja na kuongeza kipato chao kupitia ongezeko la huduma na wateja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *