MGANGA Mkuu wa Serikali Dk Grace Magembe amevitaka vituo vyote vya tiba nchini kuwa na mfumo wa huduma jumuishi badala ya kila huduma kutolewa peke yake.

Dk Magembe amesema hayo alipofanya ziara katika Kituo cha Afya Magugu kilichopo Babati, mkoani Manyara akiongozana na wadau wa Taasisi ya Kimataifa ya Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF).

“Watumishi wa kituo hiki (Magugu) kwakweli niwapongeze sana, nimeona huduma jumuishi kwa vitendo, kwakweli mmetafsiri maelekezo ya kisekta kutoka Wizara ya Afya kwa haraka sana, nimeona huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu, Mama na Mtoto, magonjwa yasiyo ya kuambukiza na huduma ngazi ya Jamii zikiwa jumuishi, hongereni sana,” amesema Dk Magembe.

SOMA: Wadau waipongeza serikali ubora huduma za afya

Amesema mwananchi anapoenda kupata huduma katika kituo cha afya ya ugonjwa mmoja ni fursa kwa watumishi na mgonjwa mwenyewe kupimwa na kupewa huduma kwa magonjwa mengine ikiwa ndio lengo la Sekta ya Afya kutoa huduma jumuishi kwa lengo la kumpunguzia mwananchi usumbufu wa kuja hospitali mara kwa mara na kugundua magonjwa mapema.

Aidha, Dk Magembe ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watumishi na wananchi kutoa elimu kwa jamii ili waweze kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote ili kupata huduma bila ya kikwazo cha fedha.

“Ukishakuwa na Bima ya afya, utaweza kugharamia huduma zote ikiwemo kumuona daktari,vipimo, dawa na huduma nyinginezo, bima ya afya itawawezesha wananchi wasio na uwezo kupata huduma,” amesisitiza Dk Magembe.

Pia, amesema Bima ya Afya kwa Wote italeta suluhisho la mambo makubwa matatu ambayo ni ufikiwaji wa huduma (accessibility), uwezo wa kugharamia (affordability) huduma pamoja na kuwahakikishia wananchi kupata huduma bora (quality) za afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *