Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, duru ya pili ya mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya ana kwa ana kati ya Iran na Marekani imemalizika mjini Geneva, Uswisi.

Jumbe za pande zote mbili zimeondoka katika ukumbi wa mazungumzo yaliyochukua muda wa takribani masaa manne, ambayo yamefanyika kwenye Ubalozi wa Oman nchini Uswisi.

Kwa mujibu wa ripoti, pande mbili za Iran na Marekani zilibadilishana maelezo kuhusu masuala ya nyuklia kupitia wapatanishi wa Oman, huku wataalamu wa masuala ya nyuklia, sheria, na uchumi wakishiriki pia.

Duru hii ya mazungumzo, ambayo ilianza yapata saa nne asubuhi leo kwa saa za Geneva, ililenga zaidi vipengele vya kiufundi vya mazungumzo hayo.

Ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi, huku upande wa Marekani ukiongozwa na Mjumbe Maalumu Steve Witkoff na Jared Kushner, ambaye ni mshauri na pia mkwe wa rais wa nchi hiyo Donald Trump.

Jumbe za nchi zote mbili zilifanya mikutano tofauti na Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman Badr Albusaidi katika Ubalozi huo wa Oman kabla ya kubadilishana maelezo kupitia wapatanishi.

Duru ya kwanza ya mazungumzo hayo ilifanyika mjini Muscat, Oman mapema mwezi huu.

Vyanzo vimeeleza kwamba katika duru hii ya mazungumzo, pande zote mbili ziliwasilisha mapendekezo ya hatua za kivitendo kuhusu masuala ya kiufundi yanayohusiana na mpango wa nyuklia wa Iran, huku Tehran ikisisitiza kuondolewa kwa vikwazo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Esmail Baghaei naye pia alithibitisha kwamba suala la kuondolewa vikwazo lilijadiliwa wakati wa mazungumzo hayo ya leo.

Wajumbe wa Iran na Marekani watarudi katika miji yao mikuu wakiktazamiwa kukutana tena hapo baadaye…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *