WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda, amesema kuwa jukumu la Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ni kuandaa na kusambaza vitabu vya shule, ikiwemo vitabu vya kiada na ziada, kwa kushirikiana na waandishi wa ndani ili kuhakikisha upatikanaji wa machapisho bora kwa wanafunzi nchini.

Amesisitiza kuwa pamoja na kuandaa vitabu vya kiada na ziada, kuna haja kubwa ya kuibua na kulea waandishi bunifu wa Kitanzania ili kuongeza upatikanaji wa vitabu vya ubora vinavyoweza kutumika shuleni na wakati huohuo kuimarisha fasihi ya Kiswahili.

Akizungumza jijini Dar-es-salaam leo Februari 17,2026 katika hafla ya uzinduzi wa vitabu vya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu, amesema lengo la tuzo hizo ni kuongeza idadi ya vitabu vinavyoandikwa na Watanzania na kuhamasisha uandishi wa kibunifu.

“Tuzo hii imepewa jina la Julius Kambarage Nyerere kwa kutambua mchango wake mkubwa katika fasihi ya Kiswahili, Mwl.Nyerere aliandika mashairi na kufasiri kazi za kifalsafa pamoja na tamthilia za Shakespeare kwa vina na mizani sahihi, hivyo kuenzi urithi wake wa kiutamaduni na kielimu,”amesema Prof Mkenda.

Akizungumzia changamoto zinazoikabili Sekta ya uchapishaji, Waziri Mkenda amesema Serikali imeweka mkakati wa kununua na kusambaza vitabu vya washindi wa tuzo hiyo shuleni na katika maktaba mbalimbali hatua inayolenga kuhakikisha soko la uhakika kwa wachapishaji na kuongeza faida kwa waandishi.

Kupitia mpango huo, uandishi unapata thamani ya kiuchumi na kijamii huku Sekta ya uchapishaji ikipewa fursa ya kukua.

Aidha, Prof Mkenda amesisitiza umuhimu wa watoto wa Kitanzania kusoma vitabu vya ndani, akieleza kuwa kutegemea vitabu vya nje pekee hakutoshi katika kujenga utambulisho wa kitaifa.

Waziri Mkenda amesema vitabu vinavyoakisi mazingira, historia na tamaduni za Tanzania vinawasaidia watoto kujitambua na kuthamini urithi wao.

Amesema uzinduzi wa vitabu vya washindi wa tuzo hiyo ni hatua muhimu katika kuhifadhi utamaduni, kuimarisha elimu na kuandaa vizazi vijavyo.

Tukio hilo, amesema, ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kuwekeza katika elimu, fasihi na kukuza sekta ya uchapishaji nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *