Mawakili nchini Morocco wamehitimisha mgomo wa wiki moja baada ya serikali kusimamisha muswada wa kudhibiti sekta ya sheria na kuunda tume iliyopewa jukumu la kuanzisha mazungumzo.

Omar Mahmoud Bendjelloun, mjumbe wa Bodi ya Kitaaluma ya Taasisi ya Mawakili wa Morocco (ABAM) amesema kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Aziz Akhannouch ameahidi kesho Jumatano “kushughulikia muswada huo, kwa ushirikiano na ABAM ili kuandaa tume mchanganyiko” ya maafisa na watendaji wa masuala ya sheria.

Serikali ya Morocco iliidhinisha rasimu ya muswada huo Desemba mwaka jana lakini sasa imeuakhirisha na kuuwasilisha bungeni ili kupigiwa kura kama ilivyokuwa imepangwa tangu awali. 

Mawakili wa Morocco wiki kadhaa zilizopita walianzisha mgomo kupinga muswada huo, ambao wameutaja kuwa tishio kwa uhuru wao.

Mapema mwezi huu maelfu ya mawakili waliovalia mavazi meusi walikusanyika katika mji mkuu, Rabat, kwa ajili ya maandamano kupinga  hatua hiyo. Hoja kuu iliyopingwa na mawakili wa Morocco ilikuwa kifungu kinachoipa mahakama mamlaka ya moja kwa moja ya kinidhamu dhidi ya mawakili. Kwa kawaida, masuala ya kinidhamu hushughulikiwa ndani na chama cha wanasheria.

Waziri wa Sheria wa Morocco pia alisema katika kikao cha Bunge mapema mwezi huu kwamba “suala hili liko mikononi mwenu na waacheni mawakili wawasilishe mabadiliko wanayotaka, nami nitajadiliana nayo. Niko tayari kutupilia mbali, kubadili au kuyafanyia mabadiliko mambo yenye madhara kwa mawakili.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *