WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba amewaagiza baadhi ya mawaziri alioambatana nao katika ziara yake mkoani Tanga kubaki mkoani humo ili kufuatilia na kutatua changamoto zilizoibuliwa na wananchi. Masuala hayo yalitokana na hoja zilizowasilishwa katika mikutano ya hadhara na wabunge wa mkoa huo pamoja na wananchi, zikigusa sekta za ardhi, mifugo, kilimo, maji, elimu na barabara.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo leo (Jumanne, Februari 17, 2026) alipokuwa akizungumza na wakazi wa Soni, Bumbuli, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye stendi ya Soni, wilayani Lushoto, mkoani Tanga. SOMA: Dk Mwigulu akutana na viongozi, wataalam Wizara ya Elimu

Amesema Serikali imepokea hoja zote zilizotolewa na wananchi na kwamba ni muhimu mawaziri husika wabaki eneo hilo ili kuzifanyia kazi kwa kina na kutoa majibu ya uhakika badala ya kuziacha bila utekelezaji wa haraka. “Nataka mawaziri wabaki hapa Tanga. Nikiendelea na ratiba yangu, wao wabaki washughulikie haya yote yaliyosemwa na wananchi ili tupate majibu na hatua za utekelezaji,” alisema.
Mapema, akijibu hoja kuhusu ubovu wa barabara wilayani Lushoto, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alisema ssan Rais Dk. Samia Suluhu Hassan tayari ameshatoa maelekezo ya kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Lushoto, ili kurahisisha usafiri na usafirishaji. Ziara ya Waziri Mkuu mkoani Tanga imelenga kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za wananchi ili kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
