Huu ni mfumo wa kisasa unaowezesha kuripoti na kufuatilia magonjwa ya mifugo kwa wakati halisi kupitia simu janja.

Magonjwa yapi yanapaswa kuripotiwa haraka?

Tanzania ina magonjwa 13 ya kipaumbele yanayopaswa kuripotiwa mara moja, ikiwemo ugonjwa wa miguu na midomo, homa ya bonde la ufa, kimeta, kichaa cha mbwa na homa ya matumbo.

Kwa kutambua umuhimu wa taarifa za wakati, Mradi wa Pamoja wa Kigoma – KJP2, umeendesha mafunzo maalum ya siku tatu kwa maafisa ugani wa mifugo kutoka halmashauri nane za mkoa wa Kigoma. Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo katika kutumia mfumo wa EMA‑i+ kuripoti milipuko kwa haraka, kutumia GPS kupata eneo sahihi la tukio, kuchangia takwimu kwenye mfumo wa kitaifa, na kuchambua taarifa kupitia dashibodi na ramani za hatari.

Washiriki pia walijifunza namna ya kutafsiri dalili za magonjwa, kutumia kanuni za ainisho la ugonjwa, kutathmini hatari, na kuimarisha ushirikiano wa One Health unaohusu magonjwa yanayoambukizwa kati ya wanyama na binadamu kama Kichaa cha mbwa, Homa ya bonde la Ufa na Homa ya matumbo

Mfugaji mkoano Kigoma nchini Tanzania akimsikiliza mtaalamu kutoka FAO Tanzania juu ya matumizi ya EMA-i+ (Event Mobile Application – improved plus) ambao ni mfumo wa kidijitali wa kudhibiti magonjwa ya wanyama.

Mfugaji (kushoto) mkoani Kigoma nchini Tanzania akimsikiliza mtaalamu kutoka FAO Tanzania juu ya matumizi ya EMA-i+ (Event Mobile Application – improved plus) ambao ni mfumo wa kidijitali wa kudhibiti magonjwa ya wanyama.

Taarifa zinafika kwa wakati

Svetlana Elieza Rwanga Daktari wa Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania anayehusika na ufuatiliaji wa magonjwa ya mifugo anasema “kupitia mfumo huu taarifa za magonjwa zinafika kwa wakati na kwa haraka na hivyo kuweza kusaidia kufanya maamuzi ya haraka ya kuzuia ugonjwa husika”

Kabla ya hapo walikuwa wanatumia njia za makaratasi ambapo taarifa ilikuwa inachukua kuanzia wiki moja hadi mbili kutoka kwenye ngazi za chini mpaka kufika ngazi za juu ambazo zinatoa maamuzi.

“Lakini kwa sasa mfumo huu toka tumeanza kuutumia, ndani ya dakika chache taarifa inakuwa imeshafika hadi ngazi ya wizara na kujua nini kinaendelea Kigoma.”

Mfumo huu ulianza kutumika nchini Tanzania mwaka 2017 walipoanza kupatiwa mafunzo  ya awali. Mwaka 2018 mafunzo yakaelekezwa kwa halmashauri 113 ambako waliona muitikio mkubwa.

Mfumo umesaidia kuharakisha maamuzi

Svetlana anasema mfano kuna wakati ugonjwa wa kichaa cha mbwa ulilipuka maeneo ya mkoa wa Kilimanjaro. “Taarifa zilifika kwa haraka sana na timu ikaundwa na tukaweza kuanza kujua ugonjwa pamoja na kuchanja na kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu ugonjwa huo.”

Kwa sasa wanahamasisha wale wote waliopata mafunzo wautumie mfumo huo na iwe ni sehemu yao ya kifaa cha kazi katika kutuma taarifa za magonjwa.

Kwa mujibu wa Joseph Nkwabi, Mtaalamu wa TEHAMA kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wao wanakusanya taarifa hizo na kuweka kwenye kanzi data. Taarifa hizo zinatumiwa na viongozi kufanya maamuzi kuhusu udhibiti wa magonjwa ya wanyama.

Mfugaji azungumza

Washiriki walienda kwenye shamba la mfugaji Ali Sahali Ali, mkazi wa kazegunga ambako mafunzo kwa vitendo yalifanyika.

Bwana Ali anasema awali alitumia siku sita kupata huduma kutoka kwa daktari wa mifugo, lakini kupitia mfumo huu anasema huduma inapatikana haraka.

“Kupitia mfumo huu kama unahitaji daktari unampata kwa wakati na utaokoa vitu vingi. Mfano akifika kama ngombe ana shida, ataangalia kwa wakati na kuepusha changamoto zaidi.”

Sadoki Kasela Afisa Mifugo kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma anakiri kuwa “mafunzo haya ya kweli kimsingi ni mazuri yameleta tija kwa sababu yatasaidia wafugaji wetu katika mkoa wetu kupata taarifa kwa uharaka zaidi kuhusiana na magonjwa na namna ya kuweza kufuatilia magonjwa haya na kuleta tija kwa wafugaji.”

Matarajio ya FAO

FAO Tanzania inasema mafunzo haya yanatarajiwa kuongeza kasi ya kugundua milipuko, kuboresha mwitikio wa haraka, na kupunguza hasara kwa wafugaji katika mkoa wa Kigoma na nchi kwa ujumla. Mikoa mingine ambayo ilipatiwa mafunzo hay oni Pamoja na Arusha, Iringa na Morogoro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *