Akizungumza na waandishi wa habari kutoka kwenye chumba cha chini ya aidhi au handaki mjini Kherson, mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF nchini Ukraine, Munir Mammadzade, amesema kuwa mji huo wa mstari wa mbele bado uko “chini ya mashambulizi ya mara kwa mara,” huku mashambulizi ya kila siku yakiharibu nyumba na miundombinu muhimu, pamoja na huduma ambazo watoto na familia hutegemea.
“Nimekuwa nikisikia milio ya mizinga mfululizo,” amesema, akizungumzia “shambulizi jingine kubwa na lililoratibiwa” ambalo linaripotiwa kuathiri miundombinu ya raia na nishati usiku kucha.
Ameongeza kuwa hospitali ya watoto ya mji huo ilishambuliwa mara nane Jumanne asubuhi.
Msichana mdogo akiwa katika makazi ya ulinzi dhidi ya bomu katika sehemu ya chini ya shule yake katika Mkoa wa Donetsk, Ukrainia. (Maktaba)
Utoto kwenye mahandaki
Kwa kuwa kuna maeneo machache sana yanayotoa hifadhi salama mjini Kherson, maisha ya kila siku ni “mapambano ya kuishi kwa watoto na familia katika eneo la mstari wa mbele” amesema, mwakilishi huyo wa UNICEF.
Amesisitiza kuwa eneo hilo “karibu lote limefunikwa kwa nyavu za kuzuia Ndege zisizo na rubani au droni, na kwamba utoto umehamia chini ya ardhi kabisa kwenye mahandaki.”
Kati ya takribani watoto 60,000 waliokuwa wakiishi Kherson kabla ya kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi tarehe 24 Februari 2022, ni takribani watoto 5,000 pekee waliobaki, na wanalazimika “kujifunza, kucheza na kulala kwenye vyumba vya chini ili kubaki salama.”
Bwana. Mammadzade ametoa maoni hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva, wakati wajadiliana kutoka Ukraine na Urusi walipokutana katika mji huo wa Uswisi kwa mazungumzo ya siku mbili yaliyoratibiwa na Marekani.
Akizungumzia chumba cha chini kilichogeuzwa kuwa kituo cha ulinzi wa watoto kinachosimamiwa na UNICEF, alikokuwa akiunganishwa, amesema kuwa “kuna watoto katika chumba cha jirani wakicheza na kushirikiana na wanasaikolojia, jambo ambalo ni la thamani sana kushuhudia katika maeneo kama Kherson kwa sababu ni nadra sana kuona watu nje.”
Wazima moto wanajibu shambulio la usiku mmoja mjini Kyiv.
Hofu ya mara kwa mara ya mashambulizi
Wahudumu wa kibinadamu wanaofanya kazi na watoto “wote wanazungumzia viwango vya uchovu ambavyo familia zinavumilia kutokana na kuishi saa 24 kwa siku katika hali ya tahadhari ya juu,” amesema.
Afisa huyo wa UNICEF amesisitiza kuwa mashambulizi yanayoathiri maeneo ya raia yanaendelea kote nchini, “ikiwemo katika maeneo ambayo hatuzungumzi sana kuyahusu,” kama vile magharibi mwa Ukraine na mji mkuu Kyiv. Amehitimisha kwa kusema kwamba “Hofu ya mara kwa mara ya mashambulizi, kujificha kwenye vyumba vya chini na kutengwa kijamii kwa mawasiliano machache kumeacha watoto wakihangaika na mazingira ya vita hivi, huku afya zao za akili na mwili zikiathirika moja kwa moja.”
Kukatika kwa umeme kila siku
Arthur Erken, Mkurugenzi wa Kanda ya Ulaya wa Shirika la Umoja wa Mataifa ;a Uhamiaji IOM, amewaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya raia, “kukatika kwa umeme sasa ndiko kunapanga maisha ya kila siku wakati familia zinapopika, watoto wanaposoma, na hospitali zinapopanga upasuaji.”
Ameongeza kuwa “Kwa halijoto kushuka hadi nyuzi -20 za Selsiasi, jamii zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa joto, umeme na matengenezo ya nyumba,” ameongeza, akisema kuwa watu waliokimbia makazi yao na wale waliorejea hivi karibuni ndio wanaoathirika zaidi.
Ukraine bado ni mgogoro mkubwa zaidi wa watu waliokimbia makazi yao barani Ulaya, amesema Bwana. Erken. Kati ya watu milioni 9.6 waliolazimika kuyahama makazi yao, milioni 3.7 ni wakimbizi wa ndani ya nchini Ukraine.
“Katika kaya moja kati ya tatu zilizohama makazi, kuna mtu anayeishi na ulemavu, na katika zaidi ya nusu ya kaya hizo, kuna mtu anayesimamia ugonjwa sugu,” amesema. “Hizi si takwimu tu, bali ni uhalisia wa kila siku unaoathiri kila uamuzi, kuanzia huduma za afya hadi kuweka chakula mezani.”
IOM ilikusanya haraka timu yake ya afya ya akili kutoa msaada kwa wale walioathiriwa na shambulio la roketi kwenye jengo la makazi huko Kryvyi Rih, Ukraine.
Mnepo pekee hauwezi kuendeleza familia
Mwakilishi huyo wa IOM amesisitiza kuwa hata baada ya miaka minne ya vita kamili, Waukraine wanaendelea kukimbia kutafuta usalama na huduma za msingi.
“Katika mwaka uliopita, zaidi ya watu 450,000 walilazimika kuhama makazi yao, wengi wao kwa mara ya pili au hata ya tatu,” amesema.
Bwana. Erken ameonya kuwa wakazi 325,000 waliorejea Ukraine wanaweza kulazimika kuhama tena katika miezi ijayo, huku zaidi ya theluthi moja yao wakifikiria kuondoka nje ya nchi tena.
“Nia ya kuondoka nchini inaonyesha mzigo wa muda mrefu wa ukosefu wa usalama, makazi yaliyoharibiwa na upatikanaji mdogo wa umeme na joto,” amesema.
“Baada ya miaka minne ya vita, ustahimilivu pekee hauwezi kuisaidia familia kuvuka majira mengine ya baridi yenye kukatika kwa umeme na baridi kali,” amesisitiza afisa huyo wa IOM.
Amehitimisha akisema “Makazi salama, nishati ya uhakika na huduma za msingi si anasa. Ni mambo ya msingi kwa ajili ya kuishi, usalama na utu wa binadamu”.