
Taarifa ya WHO iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi inasema kuwa mwaka 2023, inakadiriwa wanawake 160,000 walifariki kutokana na sababu za uzazi zinazoweza kuzuilika katika nchi zenye udhaifu wa mifumo ya afya na zilizoathiriwa vibaya na migogoro—sawa na vifo 6 kati ya wajawazito 10 duniani, licha ya nchi hizo kuchangia takribani asilimia 10 tu ya vizazi hai duniani.
Nchi zilizoainishwa kuwa zimeathiriwa vibaya na migogoro zilirekodi vifo 504 vya akina mama kwa kila vizazi hai 100,000, ikilinganishwa na 99 katika nchi zilizo thabiti zaidi.
Je ni nini visababishi?
Muhtasari huo unaunganisha viwango vya juu vya vifo vya akina mama na mifumo ya afya iliyovurugika, ukosefu wa usalama, kuhama kwa watu, pamoja na ukosefu wa usawa unaohusiana na jinsia, umri, kabila na hali ya uhamiaji.
Msichana mwenye umri wa miaka 15 katika nchi iliyoathiriwa vibaya na migogoro ana hatari ya 1 kati ya 51 ya kufariki dunia kutokana na sababu za uzazi katika maisha yake yote, ikilinganishwa na msichana 1 kati ya 593 katika mazingira thabiti.
Majawabu ya kivitendo yaliyoleta ahueni
Ripoti inaangazia majawabu ya vitendo kutoka nchi zilizohusiska kwenye mchakato, zikiwemo Colombia, Ethiopia, Haiti, Myanmar, Papua New Guinea na Ukraine.
Majawabu hayo ni pamoja na kuwafundisha wakunga wa jadi, kupeleka timu za afya za kutembea, kukarabati vituo vya afya vilivyoharibiwa, kutoa huduma ya upasuaji wa dharura wa kujifungua bila malipo au kwa gharama nafuu, kuboresha upatikanaji wa umeme, kupanga upya huduma za hospitali chini ya vitisho vya kiusalama, na kuimarisha uratibu wa ndani ili kuhakikisha mwendelezo wa huduma.
Wito wa WHO na wadau
WHO na washirika wake wanatoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji katika huduma za msingi za afya, kuimarisha ukusanyaji wa takwimu katika mazingira ya migogoro, na kujenga mifumo ya afya imara inayoweza kuhimili mishtuko na kuendelea kutoa huduma muhimu za uzazi.
“Kwa kuoanisha takwimu za vifo vya wajawazito na viwango vya udhaifu wa nchi, mashirika hayo yanasema serikali na wafadhili wanaweza kuelekeza rasilimali kwa ufanisi zaidi katika nchi zilizo hatarini zaidi na kuharakisha juhudi za kumaliza vifo vya akina mama vinavyoweza kuzuilika,” imesema taarifa hiyo.
HRP inaundwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Idadi ya Watu na afya ya Uzazi (UNFPA), la kuhudumia watoto, (UNICEF) la Mpango wa Maendeleo, (UNDP) Benki Ya Dunia na WHO yenyewe.