
LICHA ya Pamba Jiji jioni ya leo kuwa na kibarua cha kukabiliana na Alliance FC katika mechi ya hatua ya 64 Bora ya Kombe la Shirikisho (FA), kocha wa timu hiyo Francis Baraza amesema akili na hesabu zake kwa sasa ipo katika dakika 270 za Ligi Kuu dhidi ya vidogo Simba, Yanga na Azam.
Pamba itashuka kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza wakiwa wenyeji wa mechi hiyo ya kuanza msako wa tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa ya CAF msimu ujao na mara baada ya hapo itakuwa na kibarua cja kukabiliana na vigogo hivyo katika mechi za Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza alisema anawaamini wachezaji wa timu hiyo watafuata maelekezo aliyowapa ili kuhakikisha wanashinda na kutinga hatua inayofuata, lakini akili kubwa ikiwa kwenye mechi tatu ngumu za ligi zilizo katika ratiba yao.
“Tuna ratiba ngumu sana katika mechi za ligi zinazofuata baada ya kufanya vizuri tukiwa nafasi ya pili kwenye msimamo tuna kibarua kigumu dhidi ya Yanga, Azam FC na Simba kwa mujibu wa ratiba kwa mechi za ligi,” alisema Baraza raia wa Kenya aliyeongeza;
“Hii ratiba ni ngumu kwetu mechi zote tutakuwa nyumbani tunaanza na Yanga baada ya siku tatu Simba kisha siku mbili baadaye Azam hii ni ratiba ngumu sana ukizingatia tunakutana na timu bora kwenye Ligi yetu ambazo zimetoka kwenye uwakilishi wa kimataifa.”
Baraza alisema pamoja na kwamba watakuwa kwenye uwanja wa nyumbani bado wanahitaji muda wa kufanya maandalizi ya kutosha kukabiliana na timu hizo alizozitaja kuwa ni shindani kutokana na aina ya wachezaji walio nao.
“Hakuna asiye fahamu ubora wa timu hizo na baada ya kutoka kupata maumivu kimataifa kwa kushindwa kutinga hatua inayofuata zitarudi imara Ligi kuu kuja kuendelea ushindani hivyo ili kukabiliana nazo inahitajika tufanye maandalizi mazuri na kupata muda wa kupumzika,” alisema Baraza aliyewahi kuzinoa Biashara United na Dodoma Jiji na klabu kadhaa kwa huko Kenya.
“Tutafanya mpango wa kuiandikia barua mamlaka iangalie ni namna gani wataweza kutusaidia kurahisisha ugumu ulio mbele yetu kwani tunahitaji kupata matokeo mazuri ili kuendelea kujihakikishia nafasi tano bora kwenye msimamo.”