Benfica, Ureno. Jose Mourinho, ana matumaini ya kuiondoa Real Madrid katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya timu yake ya Benfica kuibuka na ushindi wa kusisimua katika hatua ya makundi.
Benfica inakutana na Real Madrid leo katika mechi ya mchujo ya kuwania kuingia hatua ya 16 bora.
Dakika za mwishoni katika Uwanja wa Estadio da Luz, Benfica walikuwa wakiongoza 3-2 dhidi ya mabingwa hao mara 15 wa Ulaya, lakini bado walihitaji bao moja zaidi ili kufuzu kwa tofauti ya mabao.
Kipa wa Benfica, Anatoliy Trubin (Kulia mwenye nguo za njano), akitoka kuupiga mpira kwa kichwa na kufunga bao katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, Jumatano, Januari 28, 2026. Picha na Mtandao
kipa Anatoliy Trubin, aliondoka langoni na kujiunga na mashambulizi katika dakika za majeruhi. Mpira wa adhabu ulipigwa kuelekea langoni mwa Real Madrid na Trubin akapaa juu kuupiga kwa kichwa na kumshinda kipa Thibaut Courtois, akiandika bao la kihistoria lililoipa Benfica tiketi ya kucheza mchujo na kwa bahati ya ajabu, wanakutana tena na Madrid.
Trubin, mwenye umri wa miaka 24, alieleza kuwa tukio hilo lilikuwa la kushangaza maishani mwake kwani hajawahi kufunga bao kama hilo. Kwa upande wake, Mourinho alisema hajawahi kushuhudia tukio la aina hiyo, akisisitiza kuwa bao la kipa katika dakika za mwisho lilimchanganya akili kwa furaha.
Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Mourinho dhidi ya Real Madrid katika maisha yake ya ukocha, jambo lililoongeza uzito wa tukio hilo.
Licha ya kuwa hawajapoteza mechi 22 katika Ligi Kuu ya Ureno, sare saba zimewaacha Benfica wakiwa nafasi ya tatu, nyuma ya vinara Porto kwa pointi saba.
Kocha wa Benfica, Jose Mourinho akishangilia bao la Kipa wake, Anatoliy Trubin alilofunga usiku wa jana dhidi ya Real Madrid katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa Januari 28, 2026. Picha na Mtandao
Akizungumzia mechi ya leo, Mourinho amesema wanakutana na timu iliyojeruhiwa, akimaanisha Real Madrid, na kuonya kuwa mfalme aliyejeruhiwa ni hatari zaidi.
Kwa upande wa Real Madrid, kichapo hicho kilikuwa pigo kubwa kwani sare tu ingewapa nafasi ya kufuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora. Badala yake walimaliza nafasi ya tisa katika hatua ya ligi kwa tofauti ya pointi moja nyuma ya Manchester City, Sporting na Chelsea.
Hata hivyo, Madrid kwa sasa wanaonekana kuimarika wakipata ushindi katika mechi tatu mfululizo za La Liga na sasa wanaongoza msimamo kwa tofauti ya pointi mbili baada ya Barcelona kupoteza jana dhidi ya Girona.
Kiungo wa Real Madrid, Jude Bellingham akiwa amekaa chini mara baada ya kupata maumivu ya msuli wa paja katika mechi ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ dhidi ya Rayo Valecano. Picha na Mtandao
Madrid itawakosa nyota wake wawili ambao ni Jude Bellingham ambaye ni majeruhi huku Rodrygo akitumikia adhabu ya kusimamishwa baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo uliopita. Mechi ya mkondo wa pili itachezwa Februari 25 katika Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Michezo mingine ya mtoano itakayopigwa leo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, itawakutanisha Galatasaray ambao watakuwa wenyeji wa Juventus, Dortmund itawakaribisha Atalanta wakati PSG wakiwa wageni wa Monaco.