
Rais wa Niger ametangaza kuanza kwa “mchakato mpya” kati ya nchi hiyo na Algeria.
Rais Abdourahamane Tiani wa Niger jana alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune mjini Algiers kwa lengo la kutangaza ujenzi wa bomba jipya la gesi.
Tebboune alisema ziara hiyo inaashiria mwisho wa “kipindi kisicho cha kawaida cha ubaridi” kati ya nchi hizo mbili.
Mwezi Aprili mwaka jana Algeria ilitungua droni kutoka Mali, nchi mwanachama wa Muungano wa Nchi za Eneo la Sahel ambao Niger na Burkina Faso pia ni wanachama.
Nchi zote tatu ziliwarejesha nyumbani mabalozi wao huko Algiers kufuatia hatua hiyo, na Algeria ikafuata mkondo.
Ujenzi wa bomba hilo jipya la gesi utaanzia Algeria hadi Nigeria kupitia katika ardhi ya Niger. Hatua za awali zinapaswa kuanza baada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Bomba la gesi la Trans-Saharan lenye urefu wa kilomita 4,000 litasafirisha gesi itakayochimbwa nchini Nigeria na kusafirisha hadi Algeria. Mipango ya mradi huo iliharakishwa mapema mwaka jana kabla ya mzozo kujitokeza kati ya Algeria na nchi za eneo la Sahel.
Baada ya mkutano wa jana huko Algiers, Rais wa Algeria ameahidi kuiunga mkono Niger ambayo inakabiliwa na mdodoro mkubwa wa kiuchumi na kuorodhesha miradi mbali katika sekta za afya na elimu.