Licha ya kuwa na hali nzuri za kilimo, uzalishaji wa ndani wa njugumawe umeshindwa kukidhi mahitaji ya kitaifa, na kwa sasa Lebanon huagiza zaidi ya asilimia 70 ya njugumawe inazotumia.
Changamoto ni pamoja na mbegu bora na ukosefu wa mbinu za kisasa za kilimo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO limechukua hatua kupatia mafunzo wakulima ili waendelee kunufaika na zao hili la mikunde lenye faida nyingi kwenye lishe na vile vile mazingira.
Bilal Abdul Karim Muhammad ambaye amepatiwa mafunzo ya kuboresha uzalishaji na uendelevu ya njugumawe au chickpeas na FAO nchini Lebanon.
Miongoni mwa wakulima ni Bilal Abdul Karim Muhammad ambaye amepatiwa mafunzo ya kuboresha uzalishaji na uendelevu.
“Mafunzo yalikuwa ya manufaa sana. Walitufundisha mambo mengi muhimu kuhusu njugumawe, ikiwemo mbinu bora za usalama kwenye chakula tunacholima, kuondoa vijidudu vinavyosababisha kuharibika na kuongeza muda wa kuhifadhi. Tumekuwa tukitumia salfati ya shaba kutibu mbegu, lakini sasa tumejifunza kutumia mbinu za bei nafuu zaidi, za vitendo, zinazoaminika na zenye ufanisi.”
Serikali ya Lebanon inalenga kuongeza uzalishaji wa ndani wa njugumawe kufikia asilimia 40 ya mahitaji ya kitaifa ifikapo mwaka 2030, kuhakikisha mazao yanakidhi viwango vya juu vya ubora na hivyo kukuza ajira zenye staha katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Mkulima Bilal anafafanua faida za njugumawe
“Njugumawe ni muhimu na zinatupatia uhakika wa kuwa na chakula. Mwishowe, mwili wako unahitaji njugumawe. Unaweza kuzila mbichi. Unaweza kuzila zikiwa zimepikwa. Zinatumika sana katika migahawa. Unapolima njugumawe nchini Lebanon, unaokoa fedha za hazina ya Lebanon badala ya kuzitumia nje ya nchi kununua chakula. Ni faida kubwa sana. Wakati huo huo, zinachangia mzunguko wa uzalishaji wa chakula nchini Lebanon.”
Chickpeas ni chanzo tajiri cha protini.
Chikelu Mba, Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uzalishaji na Ulinzi wa Mimea cha FAO anaelezea zaidi faida ya njugumawe.
“Mikunde ina kiwango kikubwa cha protini, madini na kambakamba au fibers kwa lugha ya kiingereza, kuliko aina nyingine nyingi za mazao. Na katika sehemu nyingi za dunia ambako upatikanaji wa protini ya wanyama umewekewa vikwazo kwa sababu za kiuchumi, kijamii au kidini, mikunde ndiyo chanzo pekee cha virutubisho hivi muhimu. Mikunde, kwa kuvutia, ndiyo aina pekee ya mazao, au hata mimea kwa ujumla, inayorutubisha udongo. Mikunde ina uwezo wa kunasa nitrojeni kutoka angani na kuibadilisha gesi hiyo kuwa virutubisho katika mfumo unaoweza kuendeleza mimea na mazao mengine.”