JESHI la Polisi nchini limetoa mafunzo kwa watendaji wa mtaa, vijiji na kata mkoani Geita ili washiriki kikamirifu katika kulinda amani na kuimarisha usalama wa raia na mali zao.
Chifu wa Ushirikishwaji wa Jamii, Kamisheni ya Polisi Jamii, Makao Mkuu ya Polisi Dodoma, Naibu Kamishina wa Polisi (DCP), Henry Mwaibabe ameongoza mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Geita.
DCP Mwaibabe amesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia viongozi hao kuelimisha wananchi, kuwajengea uwezo katika masuala ya ulinzi na usalama sambamba na kupambana na uhalifu.
Amesema, viongozi wa serikali za mitaa na makundi ya bodaboda wanawajibu wa kulisaidia jeshi la polisi kuhimiza jamii kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.

Awali akifungua mafunzo hayo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Herman Matemu, amesisitiza umuhimu wa viongozi na watawala wa ngazi za chini kushiriki kikamilifu kulinda amani.
Matemu amesema kuwa viongozi wa serikali za mitaa na makundi yote ya jamii inayowazunguka wao ndio walinzi wa kwanza wa amani katika maeneo yao ya utawala.

Amesema mafunzo hayo yataongeza maarifa na ujuzi katika masuala ya Polisi Jamii na ulinzi shirikishi, kubaini na kuzuia uhalifu, na kutoa taarifa za viashiria vya uvunjifu wa amani.
Mafunzo yanatolewa kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP kupitia mradi wa ‘Dumisha Amani’ yakihusisha viongozi wa serikali za mitaa na makundi ya bodaboda.
MWISHO