Kenya. Kuna wasanii wanakuja kwenye tasnia kwa kishindo, wanatoa wimbo mmoja au miwili halafu wanapotea taratibu kwenye ramani ya soko la ushindani.

Lakini wapo wachache wanaobaki, wanabadilika kulingana na nyakati na kuonyesha ubora wao katika kila kona ya sanaa. Miongoni mwao ni Sanaipei Tande jina linaloheshimika katika muziki wa Kenya na Afrika Mashariki na ambalo pia limejijengea ufalme wake kwenye uigizaji.

Sanaipei ni msanii aliyedumu kwenye muziki wa Kenya kwa muda mrefu akiwa miongoni mwa wasanii wachache waliofanikiwa kufanya kotekote muziki, filamu na hata utangazaji.

SENA 02
SENA 02

SAFARI YAKE

Jina lake halisi ni Natasha Sanaipei Tande alizaliwa Machi 22, 1985 Mombasa nchini Kenya. Ni mwimbaji, mtunzi wa nyimbo, mwigizaji, mtangazaji wa redio na mburudishaji.

Safari yake ya muziki ilianza mwaka 2004, akiwa na umri wa miaka 19 aliposhiriki shindano la vipaji la Coca-Cola Popstars (East Africa) baada ya kuhamasishwa na familia yake.

Baada ya kufaulu majaribio (audition), aliahirisha masomo yake ya famasia katika Chuo cha Mafunzo ya Tiba Kenya (Kenya Medical Training College).

Tande aliibuka mshindi wa shindano hilo pamoja na Wakenya wenzake wawili, Kevin Waweru na Pam Waithaka. Kwa pamoja waliunda kundi la muziki lililoitwa Sema na wakasaini mkataba wa kurekodi na Homeboyz Records.

SENA 05

Mashindano hayo ya Cocacola Afrika Mashariki yalizaa kikundi kwa kila nchi, Kenya (sema), Uganda (Blu-3) na Tanzania (Wakilisha, iliyoundwa na Witnesz Kibonge Mwepesi, Langa na Shaa).

Mwaka 2005, kundi la Sema lilitoa albamu yake ya kwanza iliyokuwa na nyimbo 17 iitwayo Mwewe, ikiwa na vibao kama ‘Leta Wimbo’, ‘Sakalakata’, na ‘Mwewe’. Albamu hiyo iliwapa umaarufu mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki. Hata hivyo, baadaye mwaka huo huo, kundi lilivunjika likieleza sababu kuwa ni tofauti zisizoweza kupatanishwa.

SENA 01

Baada ya kuvunjika kundi hilo, Sanaipei alianza safari ya muziki wa kujitegemea akaachia ngoma mbalimbali kama ‘Najuta’, wimbo uliogeuka gumzo kwa maudhui yake ya uhusiano na video yake iliyozua mijadala mikali mtandaoni.

Ngoma nyingine kama ‘Amina’, ‘Chaguo La Moyo’, ‘Kwaheri’, ‘Flavour’ na nyinginezo zilimtambulisha zaidi Sanaipei na kumfanya kujulikana zaidi Afrika Mashariki.

‘Najuta’ ni kati ya nyimbo zilizoweka alama kubwa kwenye kazi yake.

SENA 03

Wakati mashabiki wengi wakimfahamu kama mwanamuziki, Sanaipei aliingia pia kwenye uigizaji na kuonyesha kuwa ana kipaji kipana zaidi ya studio za kurekodi.

Ameonekana kwenye tamthilia mbalimbali kama Kina, Aziza, Varshita, Auntie Boss, The Chocolate Empire na Lulu, kila nafasi aliyopewa alionyesha uwezo wa kuingia kwenye uhusika na kuubeba kikamilifu. Si ajabu kuona mashabiki wakisema kama asingekuwa mwimbaji, bado angekuwa staa kupitia skrini.

Kati ya tamthilia alizocheza ‘Kina’ ilimpa mafanikio makubwa akanyakua tuzo ya Kalasha Awards kama Best Lead Actress in a TV Drama.

SENA 04

ANABADILIKA

Moja ya silaha kubwa ya Sanaipei ni uwezo wake wa kubadilika. Kutoka zama za CD na redio hadi enzi za mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali, ameendelea kuwepo na kushirikiana na kizazi kipya.

Amefanya kazi na wasanii mbalimbali wa Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla, akionesha kuwa yuko tayari kujifunza na kushirikiana.

Mbali na sanaa Sanaipei pia amewahi kujihusisha na shughuli za kijamii na kampeni mbalimbali zinazogusa wanawake na vijana, akitumia jina lake kama chombo cha kuleta mabadiliko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *