SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limezindua huduma ya usafirishaji wa makontena kwa kutumia Reli ya Kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR), hatua inayolenga kupanua wigo wa biashara, kupunguza msongamano bandarini na kuboresha usafirishaji wa mizigo kwenda mikoa ya kati.
Akizungumza wakati wa safari ya kwanza ya treni ya makontena kutoka Pugu jijini Dar es Salaam kwenda Ihumwa mkoani Dodoma, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Usafirishaji wa TRC, Focus Makoye Sahani, amesema treni hiyo inasafiri umbali wa takribani kilometa 420 kutoka Dar es Salaam.
Amesema uzinduzi huo unafuatia kuanza kwa huduma za usafirishaji wa abiria pamoja na mizigo mbalimbali ikiwemo mchele tangu Julai mwaka huu, pamoja na saruji inayopakiwa katika kituo cha Pugu. “Leo tumepanua wigo wa biashara kwa kuanza rasmi huduma ya usafirishaji wa mizigo ya makontena. Kama mnavyoona, treni yetu ya kwanza ya makontena kuelekea Ihumwa, Dodoma, imeanza safari rasmi na tumepata mteja wa kwanza aliyeonesha ushirikiano mkubwa,” alisema Sahani.

Treni hiyo ya uzinduzi ina jumla ya mabehewa 50 yanayobeba makontena 100. Mteja wa kwanza ni Kampuni ya GSM, iliyotoa mzigo wa awali kwa ajili ya huduma hiyo mpya. Sahani amesema shughuli za upakiaji wa makontena zimeanza katika kituo cha Pugu, huku maboresho ya miundombinu yakiendelea katika Yadi ya Malindi, eneo la karibu na Gerezani, kwa lengo la kuimarisha uwezo wa kuhudumia makontena. SOMA: TRC kutoa ajira 2,460 reli Dar – Makutopora
Ameeleza kuwa mpango huo utasaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam sambamba na utekelezaji wa maelekezo ya Mkurugenzi Mkuu wa TRC ya kuanzisha Bandari Kavu (ICD) katika maeneo ya Morogoro na Ihumwa. “Tutaweka ICD Morogoro, umbali wa kilometa 193 kutoka Dar es Salaam, ambapo wateja wanaosafirisha mizigo kwenda Mbeya na Iringa wataweza kuchukua mizigo yao huko. Pia ipo ICD ya Ihumwa,” alisema.

Amefafanua kuwa safari ya treni hadi Morogoro huchukua muda mfupi, huku mizigo inayokwenda Dodoma ikishushwa katika ICD ya Ihumwa ambayo ina eneo na miundombinu ya kutosha kwa ajili ya kushughulikia makontena kwa ufanisi. Sahani amewataka wafanyabiashara na wadau wa usafirishaji kutumia reli badala ya malori kati ya Dar es Salaam na Dodoma, akisisitiza kuwa SGR ni njia ya gharama nafuu, salama na yenye ufanisi.
Hii ni mara ya kwanza kwa TRC kutumia mabehewa maalumu ya kubeba makontena tangu kuanza rasmi huduma za usafirishaji wa mizigo kwa SGR Juni 27, 2025. Desemba 2024, TRC ilipokea jumla ya mabehewa 264 ya mizigo ya SGR, ambapo mabehewa 200 ni ya kubeba makontena na 64 ni ya mizigo ya kawaida (loose cargo).