
Dar es Salaam. Sekta ya madini inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania, ikichangia takribani asilimia 10 ya pato la Taifa na kuunganisha maelfu ya shughuli za kibiashara katika mnyororo mzima wa thamani.
Licha ya migodi mikubwa kupewa uangalizi zaidi, shughuli nyingi za kila siku zinaendeshwa na wachimbaji wa kati, wasambazaji, wakandarasi, wasafirishaji na watoa huduma wanaotegemea huduma za kifedha ili kuendesha biashara zao.
Stanbic Bank Tanzania imesema kupitia kitengo chake cha Biashara kwa Wateja wa Kati imejikita kuimarisha uwezeshaji wa biashara hizi kwa kutoa suluhisho za kifedha zinazoendana na uhalisia wa shughuli za madini, hatua inayolenga kuimarisha mwendelezo wa biashara, kudhibiti athari za hatari na kukuza ukuaji endelevu wa sekta.
Taarifa ya benki hiyo inaeleza kuwa madini ni chanzo cha pili kwa ukubwa cha fedha za kigeni nchini baada ya utalii, huku dhahabu ikiendelea kuongoza. Mbali na uchimbaji, sekta hiyo inaunga mkono mtandao mpana wa biashara za ndani zinazofanya kazi katika maeneo ya migodini, zikiwemo kampuni za vifaa, usafirishaji, uhandisi na huduma mbalimbali, ambazo mchango wake huathiri moja kwa moja tija na uimara wa mnyororo wa thamani wa madini.
Kupitia kitengo hicho, benki inatoa huduma za kifedha zilizobuniwa kwa kuzingatia uzoefu wa wachimbaji wa kati na biashara zinazohusiana na madini. Ushirikiano na wateja katika mikoa yenye rasilimali umebaini changamoto kuu zinazowakabili, zikiwemo mizunguko isiyotabirika ya malipo, gharama kubwa za vitendea kazi na matengenezo ya mitambo, changamoto za ubadilishaji fedha za kigeni pamoja na gharama za nishati.
Huduma za mikopo ya mtaji kazi zimeelezwa kusaidia biashara kuendesha shughuli za kila siku na kudhibiti mtiririko wa fedha, huku mikopo ya ununuzi wa mitambo na vifaa ikisaidia kuongeza tija, usalama na ufanisi wa kazi. Aidha, mikopo ya magari hurahisisha usafirishaji na usimamizi wa shughuli katika maeneo ya migodi.
Benki hiyo pia inatoa huduma za bima kulinda mali, wafanyakazi na shughuli za biashara katika sekta yenye hatari za kiutendaji na kimazingira, pamoja na suluhisho za kudhibiti hatari za ubadilishaji fedha kwa biashara zinazohusika na uagizaji au usafirishaji nje ya nchi.
Kadri gharama za nishati zinavyozidi kuongezeka, benki imeanza kuunga mkono matumizi ya nishati mbadala, ikiwemo umeme jua, ili kusaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa biashara za madini.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano wa kimataifa wa madini wa Mining Indaba uliofanyika Cape Town, Afrika Kusini, Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Biashara kwa Wateja wa Kati wa benki hiyo, Mollen Charles, alisema lengo la taasisi hiyo ni kutoa uwezeshaji unaoendana na changamoto halisi za biashara zinazohusiana na sekta ya madini.
“Tunataka kuhakikisha wachimbaji wa kati na biashara zinazowaunganisha wanapata huduma sahihi za kifedha katika kila hatua ya safari yao. Kwa kuunganisha mikopo ya mtaji kazi, ununuzi wa mitambo, bima na suluhisho za nishati endelevu, tunawezesha biashara kuendelea kufanya kazi, kudhibiti hatari na kukua kwa namna inayonufaisha jamii za migodini na uchumi kwa ujumla,” amesema Charles.