Dar es Salaam. Maisha ni safari, lakini muhimu ni kuwa na malengo na kupambana kuhakikisha yanatimia. Ndivyo ilivyo kwa Asha Baraka ambaye ni mwanasiasa, mwanamichezo na mmiliki wa bendi ya muziki wa dansi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ aliyeanzia mbali kupambania ndoto zake.
Hakuna ubishi kwamba, suala la kumiliki bendi nchini kwa miaka mingi limekuwa likitawaliwa na wanaume. Lakini kuna majina machache ya wanawake waliosimama imara kuanzisha na kuendesha bendi za muziki wa dansi, zikadumu muda mrefu, kwani nyingi zimekuwa zikiishia njiani kutokana na changamoto na ukiritimba wa mfumo dume.
Asha, mtumishi wa zamani wa Shirika la Bima (NIC), aliyewahi kucheza netiboli ambako aling’ara hadi akasajiliwa na timu ya netiboli ya Simba, ni shujaa. Ana historia nzuri na tamu katika eneo la uchezaji, kwani aliwahi kuvuja jasho ili kuwaburudisha Watanzania kupitia mchezo huo.
Ukiachana na hilo, ni mwanasiasa. Kwa miaka mingi amejihusisha katika masuala ya siasa akilenga kuwatumikia Watanzania kupitia njia hiyo na ni hivi karibuni alichaguliwa kuwa mbunge wa viti maalumu kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akifahamika kama ‘Iron Lady’, Asha amethibitisha kuwa wanawake wakiamua kupambania ndoto zao kwa kila hali hakuna kinachoshindikana, muhimu ni kutokata tamaa.
“Napenda kazi, nathubutu (kufanya) kila fursa inayokuwa mbele yangu. Simba sijaanza leo kuitumikia leo, nilianza kwa kuichezea netiboli zamani…,” anasema Asha, katika mahojiano na Mwananchi.
Kwa sasa mwanamama huyo ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu hiyo akiwakilisha upande wa wanachama.
Ukiachana na hilo, upande wa muziki ndiko haswa alikosimika jina lake katika miaka kadhaa kupitia Twanga Pepeta, bendi iliyowahi kuwa tishio hapa nchini.
Bendi hiyo chini ya uongozi wake ilikuwa moto ikimiliki wanamuziki wenye majina makubwa kama Ramadhan Masanja ‘Banzastone’, Msafiri Diouf. Luiza Mbutu na Ally Choki waliotikisa katika muziki wa dansi. Lakini, nyuma yao alikuwapo Asha, aliyepambana na mfumo dume kuhakikisha kwamba bendi hiyo inasimama.
Na licha ya misukosuko iliyoua bendi nyingi nchini, Twanga Pepeta chini ya uongozi wake ingalipo ikikabiliana na vita za kiuchumi, huku ikiwa inapiga muziki katika kumbi za burudani na hafla mbalimbali.
Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu kuelekea Siku ya Wanawake inayoadhimishwa Machi 8, Asha anasema hakuwahi kufikiria kukata tamaa licha ya kuwepo kwa presha na changamoto nyingi alizokutana nazo.
“Haikuwa rahisi, lakini nilijua ninachopigania. Twanga Pepeta siyo bendi tu, ni sehemu ya historia ya muziki wetu na maisha ya watu wengi. Nilijua lazima nipambane kuhakikisha inaendelea kuwepo,” anasema Asha.
Katika kipindi cha uongozi wake ameshuhudia mabadiliko makubwa ya tasnia ya muziki ikiwemo kupanda kwa kasi kwa muziki wa Bongofleva na kupungua kwa umaarufu wa muziki wa dansi, lakini hakuruhusu hali hiyo kuizima Twanga Pepeta.
Anasema changamoto kubwa aliyokutana nayo ilikuwa ni mtazamo wa baadhi ya watu kutokuamini uwezo wa mwanamke katika nafasi ya uongozi.
“Kulikuwa na wakati watu hawakuamini kama mwanamke anaweza kuongoza bendi, lakini niliamua kuonyesha kwa vitendo kuwa inawezekana,” anasema nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa netiboli akitamba na timu za Bima, Simba na Taifa Queens.
Kupitia Twanga Pepeta aliyoiasisi 1998 amefanikiwa kuwatoa kimaisha wanamuziki wengi ambao baadhi walipata darasa kupitia kwake na kumiliki bendi zao, huku wengine wakiendelea kutamba katika muziki huo, lakini nyuma wakiwa wamepitia katika mikono yake.
Juhudi zake katika jamii na mchango wake katika kukuza sanaa vimemuwezesha kupata heshima kubwa, jambo lililochangia kuaminiwa na kuteuliwa kuwa mbunge wa viti maalumu, nafasi anayodai kuwa ni sehemu ya dhamira yake ya kulitumikia taifa.
“Kuchaguliwa kuwa mbunge ni heshima kubwa kwangu. Inaonyesha kuwa kazi niliyofanya imeonekana. Nataka kuitumia nafasi hii kusaidia maendeleo ya sanaa, wanawake na vijana ili wapate fursa zaidi,” anasema mbunge huyo ambaye anaamini kwamba sanaa ni sekta muhimu inayoweza kutoa ajira na kukuza uchumi, huku akiwa na malengo pia ya kupigania maslahi ya wasanii na wadau wa sanaa kupitia nafasi yake ya uongozi.
Asha anawataka wanawake wengine wanaotamani kufanikiwa katika sekta mbalimbali wanazoamini kwamba wanaweza kutoka kimaisha, basi wafanye hivyo na kila kitu kitakwenda vyema kwao.
“Niliona fursa ya kuendeleza muziki na kusaidia vipaji vya vijana, lakini pia kuthibitisha kuwa mwanamke anaweza kuongoza. Changamoto zilikuwepo, lakini sikukata tamaa, hivyo nawahimiza wanawake wengine waamini uwezo wao na wasikubali kuwekewa mipaka,” anasema na kuongeza:
“Mwanamke anaweza kufanikiwa katika sekta yoyote ikiwa ataamua kupambana.”
Licha ya majukumu ya kisiasa, Asha bado anaendelea kuisimamia Twanga Pepeta akihakikisha kuwa inaendelea kuwa sehemu ya burudani kwa Watanzania na kuendeleza urithi wa muziki wa dansi nchini.
Leo, Asha siyo tu kiongozi wa muziki, bali ni mfano wa wanawake wanaothubutu, wakapambana na kufanikiwa kutimiza ndoto zao. Safari yake kutoka kuongoza bendi hadi kuingia bungeni ni ushahidi kuwa kwa ujasiri, uvumilivu na kujiamini mwanamke anaweza kufikia mafanikio makubwa na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii.