HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imepokea vifaa tiba vyenye thamani ya Sh milioni 183 kutoka Shirika la Operation Smile ikiwemo darubuni za upasuaji bobezi na darubini za kujifunzia ambavyo vinatarajiwa kuongeza uwezo wa hospitali katika kutoa huduma za kisasa zaidi kwa wagonjwa wanaohitaji upasuaji rekebishi.

Aidha MNH, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Shirika la Operation Smile wamesaini hati ya Makubaliano (MoU) yenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika mafunzo na utoaji wa huduma za kibingwa bobezi hususan katika eneo la upasuaji rekebishi (Microsurgery).

Makubaliano hayo yanalenga kuongeza ujuzi wa wataalamu hao, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Dk Delilah Kimambo, amesema kuwa ushirikiano kati ya MNH na Operation Smile unaakisi dhamira ya pamoja ya kuendeleza usawa katika huduma za afya kwa kuboresha utoaji wa huduma za kibingwa bobezi, hususan katika upasuaji rekebishi, pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa ndani kupitia mafunzo ya vitendo, kubadilishana ujuzi na matumizi ya teknolojia za kisasa.

Kwa upande wake, Mwakilishi Taasisi ya upasuaji rekebishi ya Operation Smile Tanzania, Dk Hamid Mandali amesema kuwa ushirikiano huo unalenga kusambaza ujuzi na mbinu za kisasa za upasuaji rekebishi kwa wataalamu wengi zaidi pamoja na kuendelea kuisaidia MNH kupitia mafunzo ya vitendo na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu, kwa lengo la kuimarisha uwezo wa ndani na kuhakikisha huduma bora, salama na zenye viwango vya juu zinawafikia wananchi wengi.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias, ambaye amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kujenga uwezo wa ndani na kuimarisha mifumo endelevu ya huduma za afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *