KIKUNDI cha Vijana Wazalendo kutoka Mamlaka ya Mji Mdogo Kibaigwa, Wilaya ya Kongwa, kimekabidhiwa magari mawili yenye thamani ya Sh milioni 75 kwa ajili ya biashara ya usafirishaji, ikiwa ni mkopo wa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri unaotengwa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Magari hayo yamekabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mayeka Simon Mayeka, aliyewapongeza vijana hao kwa nidhamu na uwajibikaji wao katika marejesho ya mikopo. Mayeka amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatamani kuona mikopo ya asilimia 10 inaleta mabadiliko chanya kwa wananchi,
Amewataka vijana hao kuyatunza magari hayo kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili yawe mfano kwa vikundi vingine na kuwahimiza kuendelea kuwa waaminifu katika marejesho ili wapate fursa zaidi za kukopeshwa. SOMA: Mradi wa Parachichi waongeza ajira kwa vijana Ngara
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, White Zuberi, amesema kamati ya fedha iliwahi kuwatembelea vijana hao walipochukua mkopo wao wa kwanza na kutokana na mwenendo mzuri wa marejesho waliwashauri kununua gari aina ya Coaster, ambalo sasa limekabidhiwa rasmi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dk. Omari Nkullo amesema mkopo huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya siku 100 ya Rais ya kutenga Sh bilioni 200 kwa ajili ya makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kiuchumi.
Aidha ameongezea kuwa halmashauri ina imani na kikundi hicho cha vijana watano kwa kuwa ni cha muda mrefu na kimeonesha weledi katika biashara ya usafirishaji, huku kikiwa na historia ya kukopa na kurejesha mikopo kwa wakati bila changamoto.
Akizungumza kwa niaba ya wanakikundi wenzake, Katibu wa Kikundi cha Vijana Wazalendo, Boaz Mbele amesema kikundi chao kilianzishwa mwaka 2015 kwa mkopo wa Sh milioni 13 waliotumia kununua gari aina ya Probox na kufanikiwa kuurejesha kwa wakati.
Katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Oktoba–Desemba), wamekopeshwa Sh milioni 75 na kununua magari mawili—Coaster na gari ndogo aina ya Wish—yatakayowawezesha kuongeza kipato na kurejesha mkopo kwa wakati.
