
Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Antananarivo UNICEF imesema kimbunga hicho, kilichopiga tarehe 10 Februari, ni cha pili kuikumba nchi hiyo ndani ya kipindi cha wiki mbili.
Ripoti za awali zinaonesha zaidi ya watu 270,000 wameathirika na zaidi ya 16,000 wamepoteza makazi yao wakiwemo karibu watoto 6,000 na takribani watoto 29,000 hawawezi kuhudhuria masomo kwa sasa.
Maeneo yaliyoathirika zaidi ni pamoja na mkoa wa Atsinanana, hasa jiji la Toamasina, jiji la pili kwa ukubwa na bandari kuu ya nchi hiyo. Maeneo ya makazi yameharibiwa vibaya, na kulazimisha familia kuishi katika makazi ya muda yaliyojaa watu kupita kiasi.
Mashirika ya misaada yanaonya kuwa hali hiyo inaongeza hatari kwa watoto, ikiwemo kutenganishwa na familia, ukatili, unyanyasaji na msongo wa mawazo.
“Familia nyingi zimepoteza makazi yao, jambo ambalo ni tukio la kuhuzunisha sana kwa watoto,” amesema Christine Jaulmes, Mwakilishi wa UNICEF nchini Madagascar.
“Kimbunga kimevuruga pia huduma muhimu wanazozitegemea maji salama, huduma za afya, ulinzi na elimu. Bila msaada wa haraka, watoto wanakabiliwa na hatari zaidi katika wiki zijazo,” ameongeza.
Huduma za maji na afya zatetereka
Kukatika kwa umeme kumeathiri mfumo wa maji katika Toamasina, na kuongeza hatari ya milipuko ya magonjwa yatokanayo na maji machafu. Hospitali zote mbili za vyuo vikuu zimeathirika, na vituo 21 vya afya vimeharibiwa. Mfumo wa kuhifadhi chanjo katika joto linalofaa umeathirika katika vituo viwili, hali inayozuia upatikanaji wa huduma za kuokoa maisha.
Mgogoro huu unakuja wakati Madagascar bado inakabiliana na madhara ya kimbunga Fytia, pamoja na mlipuko unaoendelea wa Mpox kaskazini-magharibi mwa nchi hali inayozidisha shinikizo kwa uwezo wa kitaifa wa kukabiliana na majanga.
Elimu yatikiswa na kuathirika vibaya
Sekta ya elimu imeathirika kwa kiasi kikubwa. Angalau shule 35 zimeharibiwa, madarasa 563 yameezuliwa mapaa, na madarasa 218 yamebomolewa kabisa.
Kwa maelfu ya watoto, kupoteza darasa siyo tu kukosa masomo bali pia kupoteza mazingira salama na msaada wa kisaikolojia.
Maeneo ya muda ya kujifunzia yanaanzishwa kwa ajili ya hadi wanafunzi 14,000, lakini uhaba wa fedha unatishia uendelevu wa msaada huo.
Hatua zaendelea, lakini ufadhili wahitajika haraka
Serikali inaongoza juhudi za kukabiliana na hali hiyo kupitia Ofisi ya Kitaifa ya Usimamizi wa Hatari na Maafa (BNGRC), kwa kushirikiana na washirika wa kibinadamu. UNICEF ilianza maandalizi kabla ya kimbunga kufika na kuongeza juhudi mara moja baada ya athari zake.
Vifaa vya kusafisha maji vimewafikia watu 2,400, vifaa vya WASH vimesambazwa kwa kaya 178, na vyandarua 2,000 vimetolewa kwa familia 1,000. Vifaa vya dharura vya afya vinavyoweza kuhudumia watu 60,000 kwa mwezi mmoja vimesambazwa, na hospitali zimewezeshwa kuendelea kutoa huduma.
Hatua za awali zimewezeshwa na mchango wa karibu dola 900,000 kutoka Mfuko wa Dharura wa Kukabiliana na Maafa (CERF), ulioruhusu hatua za mapema kabla ya kimbunga kufika. Hata hivyo, mahitaji yanaendelea kuongezeka.
“Tunakimbizana na muda kurejesha huduma muhimu na kuzuia mgogoro wa pili,” Jaulmes ameonya. “Tunahitaji kwa dharura dola milioni 8.4 ili kuongeza misaada ya kuokoa maisha na kusaidia urejeshaji wa mapema kwa watoto na jamii zao. Kila kuchelewa kunaongeza hatari kwa walio hatarini zaidi.”
Wakati tathmini zikiendelea, mashirika ya misaada yanaonya kuwa bila ufadhili wa ziada wa haraka, maelfu ya watoto wa Madagascar wataendelea kukosa elimu, huduma za afya na ulinzi kufuatia majanga haya ya mfululizo yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi.