Viongozi wa nchi za Afrika wametangaza mshikamano wao na watu wa Palestina na haki yao ya kujitawala.

Katika taarifa ya mwisho ya mkutano wao, wakuu wa nchi za Afrika wametangaza mshikamano wao kamili na watu wa Palestina, wakisisitiza haki yao ya kujitawala. Viongozi wa Afrika pia wamesisitiza tena upinzani wao dhidi ya jaribio lolote la kuwahamisha watu wa Palestina kwa nguvu na kuwapeleka Misri au Jordan, wakisema jambo hilo ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.

Taarifa ya Mkutano wa Viongozi wa Afrika imesema: “Tunatoa wito wa Nchi ya Palestina kupewa uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa, kwa mujibu wa matakwa ya sehemu kubwa jamii ya kimataifa.” Taarifa hiyo imeongeza: “Tunapinga kabisa jaribio lolote la kuwahamisha watu wa Palestina kwa mabavu na kuwapeleka Misri au Jordan.”

Viongozi wa Umoja wa Afrika wamesema: “Tunasisitiza mshikamano wetu kamili na watu wa Palestina na haki yao ya kujitawala na kukomesha uvamizi.” Mkutano wa kilele wa Afrika pia umeonya kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza kutokana na vikwazo vya Israel, ukieleza mshikamano wake kamili na mapambano ya kupigania uhuru ya Wapalestina na kuanzisha taifa lao huru kwenye mipaka ya 1967.

Kikao cha Umoja wa Afrika, Addis Ababa

Tamko la mshikamano la wakuu wa nchi za Afrika na watu wa Palestina katika Mkutano wa 39 wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia Februari 14 na 15, limetokana na uhusiano wa kihistoria na mitazamo ya kisiasa inayofanana. Msimamo huo haukuwa wa kinembo, bali unaakisi mtazamo wa nchi nyingi za Kiafrika kuhusu suala la Palestina kama sehemu ya urithi wa mapambano dhidi ya ukoloni na kutetea haki ya watu kujitawala na kujiamulia mambo yao wenyewe.

Mojawapo ya sababu muhimu zaidi za mshikamano huo ni uzoefu wa kihistoria wa nchi za Kiafrika na tawala za kikoloni na mapambano yao ya kupigania uhuru. Viongozi wengi wa Afrika wanaliona suala la Palestina katika mkondo ule ule wa kihistoria ambao mataifa ya Afrika yalikabiliana nao katika karne ya 20. Uhusiano huu wa kihistoria unazifanya nchi za Afrika ziliweke suala la kuwatetea Wapalestina katika ajenda yao ya kisiasa, kama sehemu ya utambulisho wa kisiasa nchi za bara hilo katika kipindi cha baada ya ukoloni. Kwa mtazamo huu, kutetea haki za Palestina kuna maana ya kutetea misingi iliyotumiwa na nchi za Afrika kwa ajili ya kupata uhuru. Nchi nyingi za Kiafrika, hasa zile ambazo zimepitia mapambano dhidi ya ukoloni na kupigania uhuru, zinajiona kwamba zina hatma moja na watu wa Palestina. Viongozi wa mapambano ya ukombozi wa Afrika kama Mzee Nelson Mandela wameunga mkono waziwazi harakati za kupigania uhuru za Wapalestina na kufananisha utawala vamizi wa Israel na utawala wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini (apartheid).

Jambo lingine ni juhudi za Umoja wa Afrika (AU) za kuthibitisha msimamo wake kama mchezaji huru na wa kujitegemea katika siasa za kimataifa. Kutoa kauli za kuonyesha mshikamano katika masuala muhimu ya kimataifa kunairuhusu taasisi hiyo kuonyesha kwamba, Afrika si uwanja wa ushindani kati ya madola ya kigeni tu, bali ina msimamo na sauti ya pamoja. Wakati huo huo, katika kipindi cha sasa ambapo ushindani umeongezeka baina ya mataifa yenye nguvu duniani kwa ajili ya kuwa na ushawishi zaidi katika bara la Afrika, kuchukua misimamo imara na ya kujitegemea kuhusu migogoro ya kimataifa kunaweza kusaidia juhudi za kuimarisha mshikamano wa kisiasa ndani ya bara la Afrika.

Katika upande mwingine, maoni ya umma katika nchi nyingi za Afrika pia yana nafasi muhimu katika msimamo huu. Katika miaka ya karibuni asasi za kiraia, makundi ya kidini na mashirika ya kijamii katika nchi mbalimbali za Afrika yameelezea hadharani uungaji mkono wao kwa Wapalestina. Watu katika nchi nyingi za Afrika wamekuwa wakifanya maandamano ya kuwatetea Wapalestina dhidi ya Wazayuni maghasibu, na kulaani uhalifu wa kutisha wa Israeli dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza, hasa katika kipindi cha vita vya mauaji ya kimbari ya Gaza.

Kwa sababu hii, kauli za kuwaunga mkono watu wa Palestina si tu kwamba zinatambuliwa kama ujumbe wa kidiplomasia unaoelekezwa nje, bali pia ni jibu linalokuja kukidhi matakwa ya maoni ya umma ya Waafrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *