“Epstein Files” ni nini?

“Epstein Files” ni mkusanyiko mkubwa wa nyaraka, barua pepe, video na picha zinazohusiana na madai ya mtandao wa kimataifa wa unyanyasaji wa kingono, biashara haramu ya binadamu na unyonyaji wa wanawake na wasichana.

Nyaraka hizi zinadaiwa kuonesha ushahidi wa vitendo vilivyofanyika kwa muda mrefu, vikihusisha watu binafsi na taasisi mbalimbali, katika mazingira yanayoashiria uwepo wa mtandao wa kihalifu wenye upeo wa kimataifa.

Mchakato wa kuzitoa hadharani unafanyika chini ya sheria iitwayo Epstein Files Transparency Act, ya nchini Marekani iliyosainiwa tarehe 19 Novemba 2025. Tarehe 30 Januari 2026, Idara ya Haki ya nchini Marekani ilitoa zaidi ya kurasa milioni 3, video 2,000 na picha 180,000.

Waathirika: Faragha yao iko hatarini

Katika taarifa yao iliyotolewa tarehe 16 Februari 2026 huko Geneva Uswisi wataalamu hao wamesema, kushindwa kulinda taarifa nyeti za waathirika wakati wa kuhariri nyaraka hizo kumeweka manusura katika hatari ya kulipiziwa kisasi, kunyanyapaliwa na kupata maumivu mapya ya kisaikolojia. Baadhi ya madhara yalitokea hata kabla kumbukumbu zilizo na taarifa nyeti kuondolewa rasmi.

Kundi la manusura hivi karibuni lilikutana na Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, likieleza hisia za kurejea katika maumivu ya awali na kile walichokiita “udanganyifu wa kitaasisi” kufuatia kusuasua kwa uwazi na uchunguzi mpana.

Wataalamu haw awa UN wamewapongeza waathirika kwa ujasiri na ustahimilivu wao katika kudai haki, licha ya gharama kubwa binafsi wanazobeba.

Makosa katika utoaji wa taarifa

Wataalamu wamesema kuwa makosa makubwa katika mchakato wa utoaji wa nyaraka yanaonesha hitaji la haraka la kuwa na taratibu maalum zinazomweka mwathirika katikati ya mchakato wa utoaji na uhariri wa taarifa.

Licha ya wingi wa nyaraka zilizotolewa, wameonya kuhusu mapungufu ya kufuata viwango vya ulinzi wa taarifa, hali inayoweza kuendeleza madhara kwa manusura. Wamesisitiza kuwa makosa ya kibinadamu hayawezi kuwa sababu ya kuathiri haki na usalama wa waathirika.

Ushahidi wa uhalifu wa kimfumo na wa kiwango kikubwa

Kwa mujibu wa wataalamu, “Epstein Files” zina ushahidi wa kushtua na unaoaminika wa unyanyasaji wa kingono, biashara haramu ya binadamu na unyonyaji wa wanawake na wasichana kwa mtindo wa kimfumo na wa kimataifa.

Vitendo vilivyobainishwa vinaweza kujumuisha utumwa wa kingono, ukatili wa uzazi, kutoweka kwa lazima, mateso, vitendo vya kinyama na vya kudhalilisha utu, pamoja na mauaji ya wanawake.

Wamesema uhalifu huo ulitendeka katika mazingira yaliyojaa ubaguzi wa rangi, rushwa, chuki kali dhidi ya wanawake, na mtazamo wa kuwafanya wanawake na wasichana kuwa bidhaa na kuwavua utu wao.

Je, yanaweza kufikia kigezo cha uhalifu dhidi ya ubinadamu?

Wataalamu wameeleza kuwa ukubwa, asili, mfumo na upeo wa kimataifa wa vitendo hivyo vinaweza kufikia kigezo cha kisheria cha uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa za jinai, uhalifu dhidi ya ubinadamu hutokea pale vitendo kama utumwa wa kingono, ubakaji, ukahaba wa kulazimishwa, biashara haramu ya binadamu, mateso au mauaji vinapofanywa kama sehemu ya mashambulizi yaliyoenea au ya kimfumo dhidi ya raia, huku wahusika wakijua kuhusu mashambulizi hayo.

Wataalamu wameonya kuwa mienendo iliyoripotiwa inaweza kukidhi vigezo hivyo na inapaswa kushughulikiwa katika mahakama zote zenye mamlaka kitaifa na kimataifa.

Uwajibikaji bado mdogo

“Hadi sasa, uwajibikaji umekuwa wa kiwango cha chini, huku mshirika mmoja tu wa karibu akiwa chini ya uchunguzi.”

Wataalamu wamezitaka mamlaka za Marekani kurekebisha mapungufu hayo haraka, kuhakikisha uchunguzi kamili, kutoa fidia na marekebisho kwa waathirika kwa madhara yote waliyopata, na kukomesha hali ya kutowajibika kwa wahusika.

“Wazo lolote la kuhitimisha mjadala kuhusu ‘Epstein Files’ halikubaliki. Hakuna aliye tajiri au mwenye nguvu kiasi cha kuwa juu ya sheria,” wamesema.

Kuhusu wataalamu hao

Wataalamu waliotoa tamko hilo ni pamoja na:

  • Reem Alsalem, Mtaalamu Maalum kuhusu ukatili dhidi ya wanawake na wasichana
  • Attiya Waris, Mtaalamu Huru kuhusu athari za madeni ya nje kwa haki za binadamu
  • George Katrougalos, Mtaalamu Huru kuhusu uendelezaji wa utaratibu wa kimataifa wa kidemokrasia na wenye usawa
  • Balakrishnan Rajagopal, Mtaalamu Maalum kuhusu haki ya makazi bora
  • Michael Fakhri, Mtaalamu Maalum kuhusu haki ya chakula
  • Ana Brian Nougrères, Mtaalamu Maalum kuhusu haki ya faragha
  • Heba Hagrass, Mtaalamu Maalum kuhusu haki za watu wenye ulemavu
  • Gina Romero, Mtaalamu Maalum kuhusu haki ya kukusanyika na kujiunga na vyama
  • Mariana Katzarova, Mtaalamu Maalum kuhusu hali ya haki za binadamu katika Shirikisho la Urusi

Wataalamu wa haki za binadamu wanateuliwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Hufanya kazi kwa hiari, si wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na hawalipwi mshahara. Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa hutoa huduma za sekretarieti kwao, lakini wataalamu hao hufanya kazi kwa uwezo wao binafsi na wako huru kutoka kwa serikali au taasisi yoyote. Maoni yao si lazima yaakisi msimamo wa Umoja wa Mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *