Aliyeacha uganga wa tiba asilia anaswa kwa wizi GeitaAliyeacha uganga wa tiba asilia anaswa kwa wizi Geita

DODOMA: JESHI la Polisi mkoani Geita linamshikilia Bahati Bushirika anayetuhumiwa kujihusisha na wizi kwa kutumia dawa za kienyeji kuwafanya waathirika wapate usingizi ili kutekeleza uhalifu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SCAP) Safia Jongo ametoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari na kueleza mhusika ni mkazi wa kata ya Nyankumbu.

Amesema uchunguzi umebaini mtuhumiwa alijiingiza kwenye matukio ya uhalifu baada ya kuacha uganga wa tiba za asili kwa madai ya kukosa wateja pamoja na kukiuka masharti ya kazi hiyo.

Amesema mtuhumiwa anadaiwa kutumia dawa za asili kuwafanya waathirika wapate usingizi kabla ya kutenda uhalifu ambapo alikamatwa katika oparesheni ya mwezi Februari 2026.

Amesema Bushirika alikamatwa akiwa na mali mbalimbali pamoja na pikipiki MC.510 EYP aina ya King Lion 150.9 rangu nyeusi ambayo alikiri kuvunja na kuiba pikipiki hiyo Januari 28, 2028.

“Mtuhumiwa aliiba pikipiki hiyo baada ya kuvunja geti la nyumba ya Limbu Nduhi ambaye ndiye mmiliki wa pikipiki hiyo, na mtuhumiwa aliwapeleka askari hadi nyumbani kwa Limbu Nduhi”.

Amesema mtuhumiwa huyo pia anatuhumiwa kwa wizi wa pikipiki MC.554 EFQ aina ya Kinglion mali ya Edward Maynga uliotokea Januari 20, 2026 katika mitaa ya Nyamalimbe.

Aidha Bushirika anatuhumiwa kuiba pikipiki MC.169 FAD aina ya SANLG mali ya Emmanuel Shabani uliotokea Januari 21, 2026 katika mitaa ya Kasamwa mjini Geita.

“Mtuhumiwa pia anadaiwa kuvunja nyumba mtaa wa Bunegezi na kuiba TV aina ya Sundar inchi 19 aliyoiuza Nyankumbu kwa shilingi laki moja”, amesema Kamanda Jongo.

Amesema jeshi la polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili (majina yanahifadhiwa) ambao wamekuwa wakijihusisha na matukio ya wizi wa simu, kompyuta na simu.

Amesema watuhumiwa hao wawili walikamatwa wakiwa na mali za wizi simu 2, aina ya Sumsung Ultra ambazo ziliripotiwa kuibiwa Geita na simu nyingine 1 zinazodaiwa kuwa za wizi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *