
Mwanadiplomasia wa Iran imeiomba serikali ya Kenya kuchukua hatua na kulipatia ufumbuzi sakata la chai la thamani ya Shilingi bilioni 2.6 za nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Balozi wa Iran nchini Kenya, Dkt Ali Gholampour katika mahojiano na gazeti la Daily Nation jijini Nairobi, ameiasa serikali ya Kenya kushughulikia faili hilo ili nchi mbili hizo ziendeleze kwa ufanisi biashara ya zao hilo baina yao.
Iran ni miongoni mwa wanunuzi 10 wakubwa duniani wa chai ya Kenya. Mnamo 2024, taifa hilo la Afrika Mashariki lilisafirisha takriban kilo milioni 13 za chai kwenda Iran, kwa thamani ya Shilingi bilioni 4.26, kwa mujibu wa takwimu rasmi za biashara.
Pamoja na kashfa hiyo, Kenya imeendelea kuwa na uhusiano mzuri wa kibiashara na Iran; kwa mfano, mwaka wa 2024, makhuruji ya Kenya kwenda Iran yalikuwa na thamani ya dola milioni 50.8 (Shilingi bilioni 6.5), ikilinganishwa na madukhuli ya thamani ya dola milioni 18 (Sh bilioni 2.3). Chai inachangia asilimia 90 ya mauzo yote ya nje ya Kenya kwa taifa hili la Asia Magharibi.
Hata hivyo, Kenya haijaiuzia Iran chai kwa kipindi cha miezi 15 iliyopita, hata baada ya kuweka makataa ya siku 60 ya kutatua mzozo huo wa mauzo ya nje ya chai mwezi Agosti mwaka jana.
Uamuzi huo ulifikiwa wakati wa Kikao cha 7 cha Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano ya Kenya na Iran (JCC) jijini Nairobi, kikiongozwa na Waziri Kiongozi wa Kenya, Musalia Mudavadi na Waziri wa Jihadi ya Kilimo wa Iran, Gholamreza Nouri Ghezelcheh.
Mvutano huo ulitokana na kashfa iliyohusisha kampuni ya Kenya ya Cup of Joe Limited, inayoshutumiwa kuagiza chai ya kiwango cha chini, kuichanganya, na kisha kuisafirisha Iran kama chai ya hali ya juu ya Kenya.
Mbali na chai, Tehran hununua nyama ya kondoo na mbuzi ($1.93 milioni) na kahawa ($1.25 milioni) kutoka Kenya. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, mauzo ya nje kutoka Kenya hadi Iran yameongezeka kwa kiwango cha asilimia 33 kwa mwaka, yakiongezeka kutoka dola milioni 11.5 mwaka 2018, hadi dola milioni 50.8 mwaka 2024.
Mwaka 2023, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya dola milioni 28.4 kwenda Kenya.