Halmashauri zapewa agizo Dira 2050, Mpango wa MaendeleoHalmashauri zapewa agizo Dira 2050, Mpango wa Maendeleo

SERIKALI imeagiza mipango na bajeti za halmashauri vizingatie utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Sospeter Mtwale alisema hayo jijini Dodoma akifungua kikaokazi cha makatibu tawala wasaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu wa mikoa na wakuu wa idara za Mipango na Uratibu wa halmashauri zote Tanzania Bara.

Mtwale ameagiza mipango na bajeti za halmashauri vizingatie matokeo, uwajibikaji na ufanisi, na utekelezaji wa vipaumbele vya Dira 2050, Mpango wa Taifa wa Maendeleo, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mipango mikakati waliyoiandaa katika maeneo yao.

Alisema kikao hicho kinafanyika wakati serikali inapanga, inaandaa mipango na bajeti ili kuhakikisha kuna matumizi bora ya rasilimali za umma ili kuongeza tija katika utoaji wa huduma.

Mtwale alisema katika kikao hicho watajadili utekelezaji wa mwongozo wa mipango na bajeti kwa mwaka 2026/27, matumizi sahihi ya mifumo ya upangaji na maboresho ya kanuni mpya ya mgawanyo wa ruzuku za serikali.

“Lengo la kanuni hiyo ni kuhakikisha mgawanyo wa rasilimali unaozingatia mahitaji halisi ya maeneo, idadi ya watu, viwango vya huduma na changamoto za maendeleo zilizopo katika mikoa na halmashauri,” alisema Mtwale.

Aidha, alisema pia watajadili Deni la Serikali katika ngazi za Mamlaka za Serikali za Mitaa hususani namna ya kuimarisha nidhamu ya matumizi, kudhibiti madeni mapya na kuweka mikakati ya usimamizi wa rasilimali fedha ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema pia watajadili utekelezaji wa mpango wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano kwa kuzingatia umuhimu wa uratibu kati ya Serikali Kuu, Sekretarieti za Mikoa na halmashauri ili kuhakikisha mipango inayopangwa inaleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi.

Mtwale ameagiza halmashauri zizingatie tafiti za kiutendaji na zibuni masuluhisho ya ndani kulingana na mazingira ya maeneo yao.

Alihimiza ziimarishe matumizi ya takwimu na zitumie matokeo ya tafiti katika kufanya uamuzi wa mipango
na bajeti ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *