Taarifa iliyotolewa leo huko Port Sudan nchini Sudan na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP imesema msafara huo ni malori 26 yaliyosheheni vyakula, dawa na vifaa vya lishe, afya, maji na elimu kwa ajili ya zaidi ya watu 130,000.
Mwanamke ambaye alikimbia vurugu katika mkoa wa Kordofan nchini Sudan anapata matibabu katika kliniki inayofadhiliwa na Umoja wa Mataifa.
Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa ni pamoja na WFP, lile la kuhudumia watoto, UNICEF, na la Mpango wa Maendeleo, UNDP.
WFP imepeleka tani zaidi ya 700 za chakula kwa watu wapatao 70,000, wakiwemo wanawake na watoto 21,000 waliopatiwa lishe maalum. UNICEF imepeleka vifaa vya kusaidia watoto 40,000, huku UNDP ikipeleka tani 70 za dawa, zikiwemo za Virusi vya Ukimwi (VVU), kifua kikuu na malaria.
Taarifa inasema msafara huo ulicheleweshwa kwa zaidi ya siku 40 kutokana na mapigano na ukosefu wa usalama katika barabara kuu ya Al Obeid–Dilling-Kadugli, na ulilazimika kutumia njia ngumu mbadala kufika jimbo la Kordofan Kusini.
Maafisa wa UN wamesema msaada huo ni muhimu kuokoa maisha, lakini wameonya kuwa upatikanaji salama na wa kudumu wa misaada unahitajika haraka.
Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande zote kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na kuruhusu misaada kuwafikia raia wote wanaohitaji bila vikwazo.
Türk atiwa hofu na mauaji ya kiraia kwa kutumia droni nchini Sudan
Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu, Volker Türk, ameonesha wasiwasi mkubwa kufuatia taarifa za kuuawa kwa zaidi ya raia 50 kwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani au droni nchini Sudan ndani ya siku mbili wiki hii pekee.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, (OHCHR) jijini Geneva, Uswisi hii leo, imemnukuu Kamishna huyo Mkuu akisema kuwa mashambulizi yalitokea kati ya tarehe 15 na 16 Februari na yalisababisha vifo vya takribani raia 57, wakiwemo watoto wasiopungua 15, katika majimbo manne ya Sudan.
Mauaji Kordofan yamefanywa na SAF na RSF
Tarehe 15 Februari, ndege isiyo na rubani inayodaiwa kuongozwa na Vikosi vya Jeshi la Sudan (SAF) ilishambulia soko la Al Safiya katika eneo la Sudari, Jimbo la Kordofan Kaskazini, na kuua watu 28 na wengine 13 walijeruhiwa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa siku iliyofuata, shambulizi lingine la droni linalodaiwa kufanywa na SAF lilipiga makazi ya wakimbizi wa ndani huko Al Sunut, Kordofan Magharibi, na kuua raia 26, wakiwemo watoto 15, na kujeruhi watu wengine 15.
Halikadhalika tarehe 16 Februari, ndege zisizo na rubani zinazodaiwa kuendeshwa na Kikosi cha wanagambo wa Msaada wa Haraka (RSF) zilishambulia shule mbili za msingi katika mji wa Dilling, Kordofan Kusini, ambapo hadi sasa idadi ya majeruhi bado haijathibitishwa.
Katika Jimbo la Sennar, droni inayodaiwa kuwa ya RSF ilishambulia hospitali ya Al-Mazmoun tarehe 15 Februari na kuua watu wasiopungua watatu, akiwemo mhudumu wa afya, na kujeruhi watu wengine saba.
Maelfu bado wamenaswa katika miji ya Kordofan, Darfur na El Fasher, ambako vita vinaendelea kupamba moto.
Darfur Magharibi taarifa za vifo na majeruhi hazijathibitishwa
Siku hiyo hiyo, katika jimbo la Darfur Magharibi, droni inayodaiwa kuwa ya SAF ilipiga ghala la mafuta ndani ya soko la eneo la Adikong, huku taarifa za majeruhi zikisubiri kuthibitishwa.
Mashambulizi dhidi ya miundombinu ya raia yakome
Türk amesema “mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia kama masoko, hospitali na shule lazima yakome mara moja.”
Na zaidi ya yote, “pande zote zinazohusika na mzozo huo zichukue hatua za haraka kulinda raia, kusitisha matumizi ya maeneo ya kiraia kwa madhumuni ya kijeshi, na kuingia katika mazungumzo ya kusitisha mapigano.”
Na hatimaye Kamishna Mkuu huyo amezitaka nchi zote, hususan zenye ushawishi, zisitishe uhamishaji wa silaha unaochochea mzozo huo na kudhoofisha ulinzi wa raia.