Chanzo cha picha, SKY NEWS ARABIA/YOUTUBE
Muda wa kusoma: Dakika 3
Majadiliano kuhusu kuunda “NATO ya Kiislamu” imekuwa moja ya hoja kuu za mazungumzo katika vyombo vya habari vya Kiarabu.
Huku Marekani ikiongeza harakati zake za kijeshi kwa uwezekano wa kuishambulia Iran, wazo la kuunda muungano wa kisiasa na kijeshi wa Kiarabu na Kiislamu limepata nguvu tena huku kukiwa na mvutano wa kieneo.
Wazo la kuunda muungano kati ya nchi za Kiislamu lilitolewa na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mnamo Septemba 2024. Alitoa wito kwa nchi za Kiislamu kuungana dhidi ya kile alichokiita wakati huo “tishio linaloongezeka la upanuzi wa Israeli.”
Mnamo Septemba 2025, Waziri wa Ulinzi wa Pakistan alitoa wito wa kuanzishwa kwa “NATO ya Kiislamu.”
Wazo hilo lilishika kasi baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya ulinzi kati ya Pakistan na Saudi Arabia mnamo Septemba 17.
Vyombo vya habari vya Kiarabu, vikinukuu safari za hivi majuzi za Bw. Erdogan nchini Saudi Arabia na Misri, vimepitia upya suala hilo na kuamini kwamba muungano mkubwa zaidi wa kijeshi unakaribia kuundwa katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.
Hata hivyo, ripoti zimekanusha, zikimtaja afisa wa Saudi, mipango yoyote ya kuunda “NATO ya Kiislamu” inayoongozwa na Riyadh na kwa ushiriki wa Uturuki na Pakistan. Ripoti zimechunguza uwezekano wa wazo hili kutokana na changamoto zilizopo
Ni nchi gani zitajiunga na muungano huu ?
Ripoti za vyombo vya habari vya Kiarabu zinaonyesha kuwa mapatano hayo yanatarajiwa kujumuisha Uturuki, Misri, Saudi Arabia, Pakistan na Indonesia.
Gazeti la Rai El Youm lenye makao yake London liliripoti kwamba safari za Bwana Erdogan huko Riyadh na Cairo zilikuwa sehemu ya mpango wa kuunda “muungano wa kisiasa na kijeshi wa Kiislamu”; muungano ambao nchi hizi tatu ndio msingi wake wa awali na ambao utaunganishwa katika siku zijazo na Pakistan (kama nguvu ya nyuklia) na Indonesia (yenye idadi kubwa ya Waislamu).
Tovuti ya “TurkPress” pia iliandika: “Kufuatia ukaribu wa kisiasa usio na kifani na uwiano wa maoni, dalili za kuundwa kwa muungano wa kikanda kati ya Misri, Saudi Arabia, na Uturuki zimeonekana kwenye upeo wa macho.”
Nini kinachoshinikiza kuundwa kwa muungano huu?
Wazo la kuunda muungano wa Waarabu na Uislamu limekuwa moja ya mwelekeo mkuu wa vyombo vya habari vya Kiarabu katika miezi ya hivi karibuni, haswa baada ya vita vya Gaza na mzozo wa siku 12 na Iran.
Tovuti ya “Europe Today” iliandika: “Changamoto na njama zinazolikabili taifa hilo la Kiarabu na Kiislamu zimefanya kuundwa kwa muungano wa kistratijia kati ya Saudi Arabia, Misri, Pakistan, Uturuki na Qatar kuwa ulazima wa dharura wa kurejesha uwiano wa madaraka na kudumisha usalama wa eneo.”
Mwanadiplomasia wa zamani wa Misri Ali Ashmawy amesisitiza katika mahojiano na Al Jazeera Mubasher kwamba muungano huu unaweza kuwa hatua ya mabadiliko katika historia ya kanda ili kukabiliana na “miradi ya kivita” ambayo inalenga kugawanya eneo hilo.
Mchambuzi wa Uturuki Ali Bekir pia aliuambia mtandao huo kwamba muungano huo utahitaji juhudi maradufu kukabiliana na “jeshi kubwa la Israel.”
Je, mtazamo wa Uturuki ni upi?
Ingawa lengo la “NATO ya Kiislamu” ilikuwa imetawala vyombo vya habari vya Uturuki kabla ya ziara ya Bw. Erdogan mapema Februari huko Riyadh na Cairo, mtazamo huo ulibadilika polepole kuelekea mada pana ya “umoja na ushirikiano wa kikanda.”
Katika mahojiano na Al Jazeera mwishoni mwa Januari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alipendekeza kuundwa kwa “jukwaa la utulivu la kikanda” ili kuongeza kuaminiana, akisema: “Hakuna utawala wa Uturuki, hakuna utawala wa Kiarabu, hakuna utawala wa Iran; hakupaswi kuwa na utawala.
Nchi za kanda zinapaswa kusimama pamoja kwa kuwajibika. Tazama jinsi gani Umoja wa Ulaya uliweza kufikia mahala ulipo leo?”
Vyombo vya habari vya serikali ya Uturuki vinakuza muundo huu kama mabadiliko katika kanda, vikiamini kuwa muungano huu utakuwa kikwazo kwa matarajio ya Israel.
Mchambuzi Johar Shulul aliandika: “Mkutano unaoonekana wa maoni kati ya Uturuki, Saudi Arabia, na Misri kuhusu masuala kama vile Iran, Syria, Gaza, na Palestina unaonekana katika sauti sawa ya taarifa zao za hivi majuzi za kidiplomasia.”
Je, ni changamoto zipi zilizo mbele yake?
Kuundwa kwa muungano huu kunakabiliwa na changamoto chungu nzima za ndani na nje.
Kwa mujibu wa Rai Al-Youm, moja ya changamoto kuu ni kwamba mikataba ya pamoja ya ulinzi kati ya nchi za Kiarabu na Kiislamu haijawahi kutekelezwa na daima imebakia “katika karatasi” na sherehe huku baadhi ya waliotia saini mikataba hii wakiingia katika migogoro ya kijeshi wakati fulani.
Wachambuzi wanaamini kwamba uratibu wa sasa kati ya Ankara, Cairo, na Riyadh bado haujafikia kiwango cha mapatano ya kimkakati ya zamani kutokana na “tofauti zilizosalia kwenye faili kadhaa, haswa masuala yanayohusiana na maendeleo ya kisiasa katika eneo hilo.”
Ali Ashmawi aliiambia Al Jazeera kwamba muungano huu hautakuwa rahisi kuunda kutokana na upinzani kutoka Israel na Marekani.
Ali Bakir pia alionya kuwa Israel haitaruhusu mpango huu kutekelezwa na kwamba harakati zake nchini Marekani tayari zimeanza kuuhujumu.
Ghadi Qandil, mtafiti katika Kituo cha Mafunzo ya Uarabuni-Eurasia, alisema, akichunguza hali za siku zijazo, kwamba “ushirikiano wa sehemu” ndio hali inayowezekana zaidi, na aliona kuwa haiwezekani kwamba harakati hii itakuwa muungano wa kitaasisi na mkubwa.