Kenya na Misri zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wao katika miradi ya maendeleo na miundombinu ya maji, ikiwemo ujenzi wa mabwawa, katika juhudi za kukabiliana na athari za ukame unaoendelea kuathiri mamilioni ya watu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Bonde la Mto Nile.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza akiwa ziarani nchini Kenya, Badr Abdelatty, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, amesema nchi yake iko tayari kuendeleza ushirikiano wa karibu na Nairobi, akihimiza Kenya kutumia fursa za ufadhili kwa miradi ya nchi wanachama wa Mto Nile ili kuimarisha usalama wa maji na kuchochea maendeleo endelevu.

Abdelatty amesema kuwa uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Misri na Kenya unapaswa kutumika kama msingi wa kuimarisha ushirikiano wa baadaye. “Tuna mahusiano ya kihistoria na inatubidi kuyatumia ili kutazama siku zijazo na kuyaimarisha zaidi kwa manufaa ya mataifa yetu,” amesema.

Aidha, ametoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji katika sekta za kilimo, dawa, nishati, ujenzi na teknolojia ya habari, akisisitiza kuwa ushirikiano wa kisiasa unapaswa kwenda sambamba na biashara, uwekezaji wa kiuchumi na hata uhusiano wa kitamaduni.

Kwa upande wake, Musalia Mudavadi, Mkuu wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, amepongeza hatua hiyo akisema Kenya imejizatiti kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na Misri kama nguzo ya utulivu wa kikanda, ukuaji wa uchumi na suluhisho za changamoto zinazoikabili Afrika.

Mudavadi amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu si tu kwa Kenya na Misri, bali pia kwa nchi wanachama wa Bonde la Mto Nile, hasa katika kuimarisha miundombinu ya maji na maendeleo ya pamoja.

Mbali na masuala ya maendeleo na biashara, mataifa hayo mawili pia yamekubaliana kuimarisha juhudi za kudumisha amani na utulivu katika Ukanda wa Pembe ya Afrika.

Victor Moturi

RFI Kiswahili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *