Magazeti ya Kenya siku ya Jumatano, Februari 18, yaliangazia maendeleo ya kisiasa nchini, huku mojawapo likiripoti uwezekano wa maridhiano kati ya Rais William Ruto na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta.

Kenyan newspapers.
Front pages for Taifa Leo and Daily Nation newspapers. Photos; screengrabs from Taifa Leoi, Daily Nation.
Source: UGC

Kwingineko, magazeti yaliripoti kuhusu zoezi linaloendelea kuhusu usajili wa Wakenya kujiunga na jeshi la Urusi.

1. Daily Nation

Gazeti hilo liliripoti kuhusu mzozo kati ya Rais William Ruto na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta.

Imebainika kuwa mzozo kati ya Ruto na Uhuru uliibuka wiki iliyopita wakati wa mkutano wa Umoja wa Afrika (AU), ambapo wawili hao walitupiana lawama katika kikao cha faragha kilichoandaliwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, kwa lengo la kuwapatanisha.

Wawili hao walikuwa kwenye mkutano uliopangwa kusaidia kurejesha amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mzozo wao katika mkutano wa Jumapili ulithibitishwa na wasaidizi, washirika na baadhi ya waliohudhuria, wakisema kuwa ulitia doa taswira ya nchi kimataifa.

Picha iliyosambaa mtandaoni ikimuonyesha Abiy Ahmed akiwa katikati ya Ruto na Uhuru ilichapishwa na upande wa rais mstaafu. Hata hivyo, upande wa Ruto haukuchapisha picha hiyo, jambo lililozua maswali.

Pia soma

Mkewe Jamaa wa Kitengela Aliyeuawa Wakati wa Mkutano wa Sifuna Asimulia Alivyofahamishwa Kifo Chake

Marais wanachama wa AU walihoji kwa nini mchakato wa amani mashariki mwa DRC umekwama, na ikaelezwa kuwa uhasama kati ya Uhuru na Ruto ndio chanzo.

Wakati Rais anahusika moja kwa moja katika juhudi za amani kwa kutuma wanajeshi mashariki mwa DRC, Uhuru yuko kwenye jopo la AU pamoja na jumuiya za kiuchumi za EAC na SADC zinazohusika na upatanishi katika maeneo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini ambako mapigano yamechacha.

Ilielezwa kuwa Uhuru anapaswa kushauriana na Ruto ili kumuarifu kuhusu hatua zilizochukuliwa na changamoto zilizopo katika mchakato wa amani mashariki mwa DRC.

Hata hivyo, ilibainika kuwa uhasama wao umechelewesha au kusitisha juhudi za amani huku raia wa mashariki mwa DRC wakiendelea kuteseka.

Ndipo Waziri Mkuu wa Ethiopia akaanza juhudi za kuwapatanisha ili kuhakikisha mpango wa amani DRC unafanikiwa.

Tofauti kali zilijitokeza wiki tatu tu baada ya Muhoho Kenyatta, ndugu wa Uhuru, kukutana na Ruto katika Ikulu ya Nairobi.

Katika siasa za ndani, Uhuru ameonekana kumuunga mkono kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, akishinikiza kufufuliwa kwa Jubilee na kumuidhinisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i kugombea urais.

Pia soma

Magazetini: Serikali Yamsaka Jamaa wa Urusi Anayewarekodi Wanawake

Uongozi wa Ruto umekumbwa na changamoto kadhaa kutokana na sera zinazodaiwa kuwaathiri wananchi, na mwaka 2024 ulikumbwa na maandamano ya Gen Z nchini.

Kuendelea kwa Uhuru kushiriki katika siasa baada ya kustaafu kunaonekana kumkera Ruto, ambaye anatafuta muhula wa pili mwaka 2027.

Chanzo kilichohudhuria mkutano huo kilinukuliwa kikisema kuwa Ruto alimkabili Uhuru kwa ushahidi, lakini rais mstaafu alikanusha kuwa anapambana na serikali ya Kenya Kwanza. Hata hivyo, alilalamika kuwa haheshimiwi na hatendewi ipasavyo kama rais mstaafu.

Ruto alimwambia Abiy kuwa alijaribu kupatana na Uhuru lakini juhudi hazikufaulu, akitaja ziara yake nyumbani kwa Uhuru Ichaweri mwaka 2024 na jitihada nyingine kupitia jamaa zake.

2. Taifa Leo

Gazeti hilo liliripoti kuhusu kuendelea kwa uandikishaji wa Wakenya kujiunga na jeshi la Urusi.

Licha ya simulizi za kutisha kutoka kwa Wakenya waliorejea kuhusu mateso yao vitani, Wakenya wengine 33 wameajiriwa na Urusi kupigana nchini Ukraine baada ya kuahidiwa mishahara mikubwa.

Idadi ya vifo na waliopotea inaendelea kuongezeka, huku ripoti mpya ya serikali ikifichua kuwa Wakenya wanane wameripotiwa kupotea au kufariki na hatima ya wengine 27 haijulikani.

Waliorejea wameripoti kuwa waliokufa huzikwa katika makaburi ya halaiki, na kuna hofu kuwa waliopotea huenda wasipatikane iwapo walifariki vitani.

Pia soma

Magazetini: Mipasuko Upinzani huku Matiang’i Akituhumiwa Kuwa Mradi wa Ruto

Ufunuo huu unatokana na taarifa ya siri kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi, iliyotolewa Februari 9.

“Tangu Januari 23, 2026, ubalozi umetambua jumla ya Wakenya 95 wanaohusika katika operesheni ya Urusi. Kati yao, 27 wamerudishwa nyumbani, wanane wameripotiwa kupotea au kufariki, 33 ni waajiriwa wapya, na 27 hawajulikani walipo,” ilisema taarifa hiyo.

Iliongeza kuwa zaidi ya Wakenya 200 wameripotiwa kujiunga hadi sasa, kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa katika ubalozi wa Kenya mjini Moscow kabla ya wao kuondoka.

Baadhi yao wanaaminika kuwa wanajeshi wa zamani wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) na Idara ya Magereza.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa baadhi ya waajiriwa wapya ni maafisa wa zamani wa vyombo vya usalama walioingia mikataba ya kijeshi kwa hiari wakifahamu wajibu wao kikamilifu.

Hata hivyo, baadhi wanaripotiwa kupanga kukimbia baada ya kupokea sehemu ya kwanza ya malipo na kisha kuomba msaada wa ubalozi ili waondoke.

Mudavadi alionya kuwa mtindo huo unaweza kuleta tishio la kidiplomasia na kuharibu sifa ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa kwa ubalozi, waajiriwa hupokea malipo ya awali ya takriban Sh1.6 milioni ndani ya wiki tatu za kusaini mkataba, kisha mshahara wa kila mwezi wa takriban Sh190,000.

Pia soma

Magazeti ya Kenya: Ida Odinga apuuzilia mbali kung’atuliwa kwa Sifuna, asisitiza angali SG wa ODM

Iwapo watajeruhiwa au kufariki, fidia ya takriban Sh1.8 milioni na Sh8.3 milioni mtawalia hujumuishwa kwenye mikataba.

Wizara bado haijathibitisha iwapo kuna Mkenya yeyote aliyepokea mshahara kamili kama ilivyoainishwa kwenye mikataba.

Mudavadi alionya Wakenya wasivutiwe na ahadi za mishahara mikubwa.

3. The Standard

Gazeti hilo liliangazia makubaliano kati ya serikali ya kaunti ya Nairobi na serikali ya kitaifa.

Baada ya uvumi, sasa ni rasmi kwamba serikali ya kitaifa itasaidia kuendesha Kaunti ya Nairobi. Ushirikiano wa Sh80 bilioni uliotiwa saini Ikulu uliwakutanisha Musalia Mudavadi na Gavana Johnson Sakaja kusimamia miradi ya maji, barabara, makazi, taa za barabarani, usimamizi wa taka na uhuishaji wa mito.

Mudavadi ataongoza kamati elekezi akisaidiwa na Sakaja, huku utekelezaji wa kila siku ukifanywa na kamati ya utekelezaji inayojumuisha makatibu wakuu na watendaji wa kaunti.

Rais William Ruto alisisitiza uhalali wa makubaliano hayo, akisema yalipaswa kutekelezwa miaka 14 iliyopita, akilalamika kuwa mji mkuu “unazama katika uchafu.”

Alisema mji mkuu lazima ufanye kazi kwa viwango vya juu vya utaratibu, miundombinu, ufanisi na utoaji huduma, si kwa wakazi wake milioni tano pekee bali pia kwa mamilioni wanaoutegemea kila siku.

Pia soma

Magazetini: Jinsi Ruto, Oburu na Wanga walivyopanga kufurushwa kwa Edwin Sifuna

Alifafanua kuwa hana nia ya kuongoza jiji hilo, bali anatekeleza wajibu wake wa kusaidia, akiahidi mabilioni kwa ajili ya taa za barabarani, maboresho ya makazi, usafishaji wa maji, upanuzi wa mifumo ya majitaka na mitandao ya barabara.

Pia alimwelekeza Waziri wa Usalama wa Ndani kuunda kikosi maalum cha Nairobi Metropolitan kuimarisha usalama.

4. The Star

Gazeti hilo liliripoti kuhusu uwezekano wa maandamano yaliyoandaliwa na muungano wa United Opposition.

Kundi hilo limeonya kuwa litaanzisha maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali ikiwa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja hatakutana nao Ijumaa.

Hii inafuatia siku chache baada ya polisi kuvuruga mkutano wa ODM uliokuwa ukiongozwa na Edwin Sifuna, ambapo mtu mmoja alifariki.

Likiongozwa na kiongozi wa Democracy for Citizens Party Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kundi hilo linasema linataka taarifa kuhusu uchunguzi wa mashambulizi yanayodaiwa kuchochewa na polisi hapo awali.

Seneta wa Makueni Dan Maanzo alithibitisha kuwa walitoa notisi rasmi wakimtaka Kanja achukue hatua, akisema watarudi na wananchi Ijumaa na kutoa ratiba ya maandamano ya nchi nzima.

Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa alidai kuwa IG na manaibu wake hawakuwepo ofisini walipowatembelea, akisema wanaamini wameagizwa kutokutana nao.

Pia soma

Magazeti ya Kenya, Feburuari 12: Ndani ya mkutano mrefu wa ODM faraghani ulioafikia kumtimua Sifuna

Alisisitiza kuwa wanamtaka IG Kanja mwenyewe awajibike na kwamba hawatasita hadi maafisa wote wanaodaiwa kukiuka haki za binadamu wawajibishwe.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *