Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, ameiagiza Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) mkoani hapa kufanya ziara maalumu katika halmashauri zote ili kujiridhisha na kutambua maeneo yaliyotengwa kwa fursa za uwekezaji.
Malisa ametoa agizo hilo Februari 17, 2026, wakati akifungua kikao cha kampeni ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani mkoani Mbeya, kilichowakutanisha wadau wa sekta binafsi na kuratibiwa na Mamlaka ya Uwekezaji wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza).
Amesema Serikali tayari imeainisha maeneo ya uwekezaji katika halmashauri mbalimbali, hivyo TCCIA inapaswa kuyatembelea na kuyathibitisha ili kuongeza uelewa na kuvutia wawekezaji wa ndani.
“TCCIA nendeni mkajiridhishe na maeneo ya fursa za uwekezaji. Ni vigumu kuamini kwa kusikia tu, lazima kuyaona kwa macho. Hata mimi nitafanya ziara katika halmashauri zote,” amesema Malisa.
Alisisitiza ushiriki mkubwa wa TCCIA katika kuhamasisha uwekezaji wa ndani na kuisukuma Serikali kutoa ushirikiano stahili ili kuvutia wawekezaji wazawa, tofauti na dhana iliyozoeleka kuwa fursa hizo ni za wageni pekee.
Malisa amesema Mkoa wa Mbeya una wajasiriamali wengi wenye mwamko wa kibiashara, hivyo elimu ya uwekezaji inahitajika ili kupanua wigo wa uchumi na ajira. Pia aliiagiza Tiseza kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi ya kimkakati, ikiwamo ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Mbeya hadi Tunduma mkoani Songwe.
Katika hatua nyingine, amewataka wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani humo kushiriki kikamilifu vikao vya kampeni ya kuhamasisha uwekezaji ili kubainisha maeneo yaliyotengwa na kutekeleza maelekezo ya Serikali.
“Wakurugenzi ni watu muhimu katika kubainisha maeneo ya uwekezaji. Ushiriki wao ni mdogo, lakini lengo la Serikali ni kuwezesha Mkoa wa Mbeya kufikia asilimia 70 ya uwekezaji nchini,” amesema.
Meneja Uhamasishaji na Uwekezaji wa Tiseza, Daud Riganda, amesema kupitia uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Tanzania imefanya mageuzi ya sera, sheria na mifumo ya kiutawala yaliyoongeza imani ya uwekezaji wa ndani na kimataifa.
Amesema kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani inalenga kubadili mtazamo uliodumu kwa muda mrefu kuwa uwekezaji ni wa wageni pekee, akisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika uwekezaji, uzalishaji na umiliki.
Kwa mujibu wa Riganda, Mkoa wa Mbeya una fursa nyingi kutokana na jiografia yake, ikiwamo kilimo cha kimkakati (mboga mboga), viwanda vya kusindika mazao, madini, utalii na uvuvi, pamoja na miundombinu kama Uwanja wa Ndege wa Songwe.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa (Uchumi na Uzalishaji), Anna Mwambene, alisema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha wadau wanatambua na kutumia fursa za uwekezaji ili kuchochea uchumi, ajira na kufikia malengo ya Serikali.
Akizungumza kwa niaba ya wadau, mkulima na mfanyabiashara wa ndizi, Thomas Jackson, amesema utoaji wa elimu kwa makundi ya wazalishaji ni muhimu ili kufanikisha uwekezaji, hususani katika uanzishaji wa viwanda vidogo vya kusindika mazao.