SERIKALI imezindua awamu ya kwanza ya mradi wa kusambaza nishati safi ya kupikia katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100.
Awamu hiyo inahusisha shule 52 za sekondari na chuo kimoja cha Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika mikoa 18 ya Tanzania Bara.
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba alizindua mradi huo katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa wilayani Kondoa, Mkoa wa Dodoma.
Mradi huo ni sehemu ya mpango wa kuunganisha miundombinu ya nishati safi ya kupikia katika taasisi 453 wenye thamani ya Sh bilioni 25.8. Gharama zote zinagharimiwa kwa asilimia 100 na serikali kupitia Wakala ya Nishati Vijijini (REA).
SOMA: Serikali kuwaunga mkono wadau nishati safi
Makamba amesema mradi huo unahusisha usimikaji wa mifumo ya gesi ya LPG, ufungaji wa majiko banifu na usambazaji wa mkaa mbadala katika taasisi 453.
Alisema katika awamu ya kwanza, taasisi 53 zitanufaika na awamu ya pili ikihusisha taasisi 400 zilizopo katika mikoa yote nchini.
“Ili mradi huu uwe endelevu, nitoe wito kwa serikali za mitaa, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Tamisemi (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) kusimamia mifumo iliyofungwa ili iwe endelevu, suala litakalohamasisha jamii kuiga mfano wa taasisi za umma kuhamia katika nishati safi ya kupikia,” alisema Makamba.
Ameitaka sekta binafsi kuona na kuchangamkia fursa iliyopo katika uzalishaji na usambazaji wa nishati safi ya kupikia ili kuongeza upatikanaji na kupunguza gharama kwa wananchi.
Ameitaka REA kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo ya minada, stendi na masoko, kwani tafiti zinaonesha kuwa kuna minada ya awali na upili ipatayo 13,763 pamoja na masoko ya samaki yapatayo 1,229 nchini, yanayopaswa kufikiwa kutokana na kuhudumia kundi kubwa la wananchi.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ambaye ni Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia, Nolasco Mlay alisema mradi huo utapunguza matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi za elimu, kuchangia uhifadhi wa mazingira, kuboresha afya na usalama wa wapishi pamoja na kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa shule.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Jones Olotu alisema takwimu zinaonesha matumizi ya nishati isiyo safi yamesababisha takribani hekta 46,606 za misitu kuharibiwa kila mwaka kwa ajili ya kuni na mkaa.
Olotu alisema watu zaidi ya 33,000 wanafariki kutokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia na wanawake na watoto wa kike kutumia saa nne hadi nane kutafuta kuni, jambo linaloathiri muda wa shughuli za maendeleo.
