
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Mwakilishi wa Kidiplomasia wa Mfuko wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN) Kanda ya Afrika Mashariki Amin Mawji aliyefika Ikulu Zanzibar tarehe 18 Februari 2026 akiambatana Mratibu wa AKDN Zanzibar Rahim Bhaloo.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mfuko wa Aga Khan hususan katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. SOMA: TADB yaendelea diplomasia ya uchumi kupitia kilimo

Rais Dk. Mwinyi ameushukuru Mfuko wa Aga Khan kwa mchango wake mkubwa Zanzibar ikiwemo huduma za afya, programu za mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji katika sekta mbalimbali, pamoja na uwekezaji na misaada katika sekta ya elimu.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huu kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar akibainisha kuwa juhudi za pamoja kati ya Serikali na wadau wa maendeleo zina mchango mkubwa katika kuharakisha ustawi wa kijamii na kukuza uchumi wa eneo hilo.
