
Kila siku inapochomoza, idadi ya vijana wanaotumia muda wao mwingi vijiweni inaongezeka kwa kasi. Hali hii inachangiwa na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa ni ukosefu wa ajira. Uchunguzi unaonyesha kuwa wapo vijana A kujiajiri lakini wakakwama kutokana na changamoto kadhaa.
Tatizo la ajira si la Zanzibar pekee; ni changamoto inayoikumba dunia nzima, hata katika mataifa yanayojitahidi kupambana na umasikini.
Hata hivyo, kwa Zanzibar, licha ya kauli za kuwepo kwa ahueni, bado kuna kazi kubwa ya kufanya kutafuta suluhu ya kudumu. Kuongezeka kwa vijiwe vyenye vijana wasio na ajira ni kielelezo cha wazi cha ukubwa wa tatizo hili.
Sababu za hali hii ni nyingi. Moja ni ongezeko kubwa la idadi ya watu mijini na vijijini. Wakati wa Mapinduzi ya Januari 12, 1964, idadi ya watu Unguja na Pemba ilikuwa takribani 290,000.
Leo hii imezidi milioni mbili, ongezeko la zaidi ya mara saba. Wakati huo huo, ukubwa wa visiwa haujaongezeka; badala yake, maeneo ya kilimo yanaendelea kupungua kutokana na kuongezeka kwa makazi na athari za bahari kula ardhi katika baadhi ya maeneo.
Aidha, mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri dunia kwa sasa yameathiri sekta ya kilimo, ambayo ni mhimili muhimu wa ajira. Upungufu au kutokuwepo kwa mvua za kutosha kunafanya uzalishaji kupungua na hivyo kupunguza fursa za ajira. Vilevile, ukuaji wa teknolojia umebadilisha soko la ajira. Kazi zilizokuwa zikifanywa na watu wanne sasa zinaweza kufanywa na mtu mmoja au mashine. Baadhi ya ajira zimepotea kabisa, kama vile ofisi za kuchapa barua kwa mashine za taipu au maduka ya kuuza kanda za video.
Pamoja na changamoto hizo za kimazingira na kiteknolojia, zipo dosari zinazoweza kurekebishwa ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wetu. Miongoni mwao ni kuruhusu baadhi ya kazi zinazoweza kufanywa kwa ufanisi na wazawa au Watanzania Bara kufanywa na wageni.
Hivi karibuni kupitia mijadala katika Baraza la Wawakilishi, uongozi wa Kamisheni ya Utalii umekemea mwenendo wa wageni kusajili kampuni kwa hila ili kufanya kazi ambazo kisheria zimetengwa kwa wazawa. Suala hili halipaswi kuchukuliwa kwa mzaha. Linahitaji uchunguzi wa kina katika sekta zote na hatua madhubuti za kuziba mianya ya udhaifu.
Sheria zilizopo zitekelezwe kikamilifu, na adhabu kwa wanaozivunja zichukue mkondo wake bila upendeleo. Onyo na matamko yameshatolewa; kinachohitajika sasa ni utekelezaji wa vitendo.
Idara ya Kazi ina wajibu wa kufuatilia kwa karibu ajira katika sekta mbalimbali na kuhakikisha nafasi zilizopo, hasa katika sekta zinazokua kama utalii na viwanda, zinawanufaisha vijana wa Zanzibar.
Kadhalika, Idara ya Uhamiaji ihakikishe vibali vya makazi na ajira vinatolewa tu pale panapothibitika kuwa kuna uhitaji wa kweli wa ujuzi usiopatikana kwa wazawa.
Hakuna mantiki ya kuruhusu wawekezaji kuleta wafanyakazi kutoka nje kwa kazi ambazo vijana wetu wanaweza kuzifanya kwa ufanisi, kama upishi, usafi wa vyumba, mapokezi au uongozaji watalii. Vivyo hivyo, Wizara ya Biashara inapaswa kuwa makini katika utoaji wa leseni kwa wageni wanaotaka kufanya biashara ndogo ndogo kama mikahawa ya vyakula vya haraka, mitumba au uuzaji wa vifaa vya ujenzi na umeme, biashara ambazo wazawa wanaweza kuzimudu.
Serikali imetoa uhuru kwa vyama vya wafanyakazi kulinda haki za wanachama wao, ikiwamo ajira kwa vijana. Hata hivyo, jukumu hili halionekani kutekelezwa kwa ufanisi unaotarajiwa. Ni wakati wa vyama hivyo kufuatilia mikataba na ajira kwa karibu ili kuhakikisha nafasi zilizopo zinajazwa na wazawa.
Juhudi zinazofanyika kila mwaka katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi, Mei Mosi, za kudai nyongeza za mishahara na maslahi bora, zinapaswa pia kuelekezwa katika kulinda ajira zilizopo visiwani.
Ni wakati wa kuacha maneno mengi na kuchukua hatua. Kwa kutumia ipasavyo sheria zilizopo na kuziba mianya ya udhaifu, tunaweza kupunguza tatizo la ajira linalowakabili vijana wetu na kulinda mustakabali wao.